Wednesday, March 28, 2012

MCHUNGAJI ALIYEGEUKA MUUAJI-SEHEMU YA MWISHO


Muuaji John Nelson Canning

ILIPOISHIA..........

Ni katika kipindi hicho ambapo ujenzi wakanisa hilo ulipoanza ndipo mauaji ya Gleese na mkewe yalipotokea. Polisi wa upelelezi waliona ni vyema wakaanza upelelezi wao kwa kuangalia vyanzo vyake vya mapato pamoja na matumizi.

ENDELEA KUSOMA HAPA.................

Katika upelelezi wao ndipo walipokuja kugundua kwamba ndani ya wiki moja tangu mchungaji Canning apewe jukumu la kusimamia akaunt za familia ya Gleese ndipo alipolipa deni lake lote la manunuzi ya lile ghala aliloligeuza kuwa kanisa, na baada ya hapo akaanza matumizi makubwa ya fedha kwa kununua nyumba mbili zenye thamani ya dola 83,000, na wakati huo huo alianza upanuzi wa nyumba aliyokuwa akiishi kwa kuifanya kuwa ya kisasa zaidi. Kwa muda mfupi akaunti za familia ya Gleese ilikuwa imekauka ikiwemo akaunti yao nyingine ya akiba iliyokuwa na kiasi cha dola 16,000, zilikuwa zimetoweka kusikojulikana.

Polisi wa upelelezi walipowahoji marafiki wa familia ya Gleese, walidai kwamba wiki moja kabla ya kuuwawa kwao mke wa Gleese bibi Hazel Gleese alianza kumtilia mashaka mchungaji Canning kuhusiana na namna anavyosimamia fedha zao. Bi Hazel aliwaambia majirani zake kwamba anapanga kwenda katika benki jijini New York walipoweka fedha zao ili kuonana na meneja wa benki ili kupata taarifa ya fedha zao kwa mwaka mzima, lakini ikiwa imebaki siku chache kabla ya bi Hazel kwenda benki wakakutwa waameuwawa na hiyo ilitokea baada ya familia hiyo kugundua kwamba mchungaji Canning alikuwa ameghushi sahihi zao na kujiandikia hundi ambapo alikuwa akijilipa yeye mwenyewe.

Polisi wa upelelezi waliamua kuhamishia upelelezi wao katika benki hiyo iliyoko katika jiji la New York ambapo walikwenda na zile taarifa za benki (Bank statements) walizozikuta zimesambaa sakafuni baada ya mauaji yale kutokea. Hata hivyo mapaka kufikia hapo, bado polisi walikuwa hawajpata ushahidi wa kina wa kumfungulia mchungaji Canning mashitaka kuhusiana na mauaji ya ajuza wale.
Msemaji mwingine wa timu hiyo ya upelelezi wa Robert Glick alisema kwamba wanao ushihidi mwingine kutoka kwa raia mwema anaeishi jirani na kanisa la mchungaji Canning ambae alibainisha kwamba siku ile yalipotokea mauaji alimuona mchungaji huyo akienda na kurudi mara kwa mara kwenye shimo la taka lililoko jirani na kanisa hilo ambapo inasemekana kwamba huenda alikuwa antafuta namna ya kuizika miili ya ajuza wale. Askari wa upelelezi walipoenda kuchunguza nyumbani kwa mchungaji huyo walikuta saa ya mkononi ambayo ilikuwa na matone ya damu, damu hiyo ilipochunguzwa aktika maabara ilikuja kugundulika kuwa ilikuwa ni ya Leo Gleese. Mpaka kufikia hapo Polisi wakawa na uhakika kwamba sasa wamembaini muuaji wa Leo na

Hazel Gleese, nae si mwingine bali ni Mchungaji John Nelson Canning.
Siku chache baada ya kuongoza mazishi ya ajuza wale mchungaji Canning alikamatwa na kushitakiwa kwa mauaji ya ajuza wale. Katika kesi hiyo mchungaji Canning alikiri kuwa aliwauwa Leo na mkewe Hazel Gleese kwa kuwapiga kwa kitu kizito na kisha kuwanyonga usiku wa Januari 3, 1995, hiyo ilitokea baada ya kuwa amebanwa na ajuza hao kuhusiana na namna alivyotumia fedha zao huku wakimuonyesha taarifa ya benki inayoonyesha kwamba alijiandikia hundi na kujilipa yeye mwenyewe.

Mnamo Februari 1996 mchungaji John Nelson Canning alipatikana na hatia ya kuhusika na mauaji ya Leo na Hazel Gleese ambapo alihukumiwa kifungo cha maisha jela bila ya uwezekano wa kupata msamaha wa kifungo cha nje (Parole). Mara baada ya kusomwa hukumu hiyo msemaji wa Polisi Phil Ramer aliwaambia wandishi wa habari kwamba hili ni tukio ambalo hatakuja kulisahau katika maisha yake.

Kwa maneno yake mwenyewe alisema “ni vyema watu wakawa waaminifu, ni jambo la kushangaza kukuta mchungaji ambae ameaminiwa na waumini wake kisha anakuja kuwaua baadae kwa sababu ya pesa”

*********************MWISHO*******************

Tuesday, March 27, 2012

MCHUNGAJI ALIYEGEUKA MUUAJI



Muuaji John Nelson Canning

Mnamo January 3, 1995 mchungaji mmoja aitwae John Nelson Canning alikwenda katika kituo cha Polisi cha mji mdogo wa Sebring ulioko katika jimbo la Florida nchini Marekani na kutoa taarifa juu ya mauaji ya vikongwe wawili mtu na mkewe Bwana Leo na bibi Hazel Gleese.
Mchungaji huyo aliyekuwa na umri wa miaka 59 wakati huo aliwaeleza Polisi kwamba aligundua mauaji hayo baada ya kuwa amewatembelea nyumbani kwao kama ilivyo kawaida yake ya kuwatembelea waumini wake na kukuta miili ya vikongwe hao ikiwa imelala sakafuni kwenye dimbwi la damu.

Mchungaji Canning aliendelea kuwaeleza Polisi kwamba bwana na bibi Gleese ni waumini wa siku nyingi katika kanisa la Fountain of life ambalo yeye ni muanzilishi wake. Mchungaji huyo alibainisha kwamba katika kipindi cha miaka ya karibuni alikuwa ni muangalizi wa vikongwe hao ambao hawakubahatika kupata watoto katika maisha yao ya ndoa ambapo waliamua kumuasili mchungaji huyo na kumfanya mtoto wao na hivyo akawa anawaita Baba na Mama. Mara baada ya kupata taarifa hizo Polisi walikimbilia kwenye eneo la tukio na kukutana na hali ya kutisha katika eneo la tukio ambayo hawatakuja kuisahau.

Kwani waliukuta mwili wa Bibi Hazel Gleese ambae alikuwa na umri wa miaka 90 wakati huo umelala jikoni ukiwa umetapakaa damu. Na mwili wa mumewe leo Gleese nao pia ulikutwa ukiwa umeegemea ukuta wa chumbani. Wote walikuwa wanaonyesha kwamba walikuwa wamepigwa na kunyongwa. Katika eneo ambalo miili ya ajuza wale ililala polisi wa upelelezi walikuta pia baadhi ya nyaraka za kibenki zikiwa zimesambaa pale sakafuni huku baadhi ya nyaraka hizo zikiwa zimelowana kwa damu, pia kulikuwa na dalili zote kwamba bibi kulikuwa na purukushani za kupigana kati ya bibi Gleese na mtuhumiwa au watuhumiwa wa mauaji. Siku ya mazishi ya maajuza hao umati mkubwa wa watu wa mji wa Sebring walihudhuria mazishi hayo yaliyoongozwa na mchungaji John Nelson Canning.
Akiongoza mazishi hayo mchungaji Canning, kwa maneno yake mwenyewe alisema “Miongoni mwenu mlikuwa marafiki wa muda mrefu wa baba na mama yangu hawa, lakini ninayo mashaka kwamba yupo mtu yeyote aliyekuwa karibu na na familia hii zaidi yangu na mke wangu”
Huku akitokwa na machozi, mchungaji huyo aliendelea kusema “Najivunia familia ya ajuza hawa kuniomba waniasili (Adopt) niwe mtoto wao, na nilijivunia kuwaita baba na mama kama wazazi wangu”


Familia ya Gleese haikubahatika kupata watoto katika maisha yao ya ndoa ndio sababu waliamua kuwaasili Canning na mkewe Judy hapo mnamo mwaka 1994. Hata hivyo wakati wa mazishi hayo bado Polisi wa upelelezi walianza kumtilia mashaka mchungaji huyo kwa kumhusisha na mauaji ya ajuza wale.

Polisi hao wa upelelezi walianza kumtilia mashaka mchungaji Canning tangu siku ile ya kwanza alipokwenda kutoa taarifa ya kutokea kwa mauaji ya ajuza wale ambao aliwachukulia kama wazazi wake. Akiandikisha maelezo yake Polisi namna alivyogundua mauaji ya Bi hazel na bwana Leo Gleese, Canning aliwaeleza Polisi akiwa katika hali ya kawaida kabisa. Kwa maneno yake mwenyewe Canning alisema “kwa kweli niligundua mauaji hayo jana asubuhi”

Polisi wa upelelezi walistushwa na habari hizo, kwani kwa mujibu wa maelezo yake ilionyesha kuwa miili ya Hazel na Leo Gleese ilikuwa imelala pale sakafuni kwa masaa 24 tangu kuuwawa pamoja na kuwa mchungaji Canning alifahamu kuhusu kutokea mauaji tangu jana asubuhi. Alipoulizwa kwamba kwa nini hakutoa taarifa mapema, mchungaji Canning alidai kwamba aliogopa kutoa taarifa kwa sababu hapakuwa na shahidi mwingine zaidi yake, hivyo aliogopa kuwa mtuhumiwa wa kwanza kuhusishwa na mauaji yale.

Kwa maneno yake mwenyewe Canning alsema “ Niliingia ndani na kustushwa na mauaji yale, nilichanganyikiwa na kufunga mlango kisha nikaondoka kwani niliogopa kutoa taarifa za vifo hivi kwa kuhofia kwamba nitahusishwa navyo mpaka leo ndio nikakata shauri nije nitoe taarifa” Mchungaji Cunning aliendelea kuwaambia polisi wa upelelezi kwamba akiwa ameshikwa na kihoro alishinda kutwa nzima akifikiria jinsi atavyotoa taarifa za vifo vile. Alipoulizwa kwamba siku hiyo ya kihoro aliitumia akiwa wapi, Mchungaji Canning aliwashangaza polisi kwa kuwaambia kuwa alishinda ufukweni mwa Bahari akiwa na marafiki zake na kisha usiku wakaungana pamoja kwenye mghahawa mmoja kwa ajili ya kupata mlo wa usiku.

Kwa ujumla maelezo ya Mchungaji Canning yalikuwa yanatia mashaka kwani Polisi wa upelelezi walibaki wakijiuliza kuwa, hivi hiyo ndio tabia ya mtu aliyeshuhudia mauaji ya kikatili ya watu ambao aliwafanya kuwa wazazi wake? Kuanzia hapo Polisi wa upelelezi walianza kumuhoji Mchungaji Canning kwa makini zaidi. Msemaji wa Polisi Phil Ramer akizungumza na waandishi wa habari alisema “Kama inamchukuwa mtu siku nzima kutoa taarifa za vifo vya watu wanaomuhusu waliouwawa kikatili, hiyo haiwezi kuwachukuwa wanasayansi wa kutengeneza Roketi kugundua kwamba muuaji nai nani”

Kwani kwa jinsi Canning anavyojieleza, ndivyo anavyozidi kudhihirisha kwamba kuna jambo analificha kuhusiana na mauaji hayo, alibainisha askari wa upelelezi anaeongoza timu ya wapelelezi wanaochunguza mauaji hayo Sajent Steven Carr. Kwa muda mfupi wapelelezi wa polisi walikuja kugungua kuwa Mchungaji Canning na Familia ya Gleese walikuwa na uhusiano wa karibu sana.

Historia inaonyesha kuwa awali Mchungaji Canning alikuwa ni ni Mchungaji wa kanisa moja lilipo katika mji wa Maine lakini baadae akaja akahamia katika mji wa Sebring na kuanzisha kanisa lake mwenyewe aliloliita Fountain of life hapo mnamo mwaka 1980. Miongoni mwa waumini wa kanisa hilo kulikuwa na wazee zaidi ya 50 ambao walikuwa ni wafuatiliaji wazuri wa mahubiri ya mchungaji Canning kupitia luninga kabla ya kujiunga na kanisa hilo.
Hapo ndipo kwa mara ya kwanza ilipotokea Leo Gleese mhasibu mstaafu na mkewe Hazel mwana mitindo wa zamani kujuana na mchungaji Canning.

Ni katika kipindi hicho ndipo familia ya Gleese ilipomuasili mchungaji Canning na mkewe na kuwaamini kiasi cha kuwafanya kama watoto wao ambapo kutokana na hali zao kuwa dhaifu kwa sababu ya uzee walimpa mamlaka ya kumiliki akaunti zao na kuwa mshauri wa familia hiyo katika maswala ya kifedha, kosa ambalo lilikuja kuwagharmu maisha yao. Pia polisi wa upelelezi walikuja kugundua kwamba mchungaji Canning hakuwa ameaminiwa na familia ya Gleese tu bali pia waumini wengi katika kanisa lake walimuamini na kumfanya mshauri wao wa maswala ya kifedha.

Pia wapelelezi hao wa polisi walikuja kushangaa baada ya kugundua kuwa kw takribani miaka 15 kanisa la Fountain of life lilikuwa likiendeshwa katika ghala chakavu alilolinunua mara baada ya kuhamia Sebring, na katika kipindi cha miaka kadhaa mchungaji Canning alikuwa akichangisha fedha kwa waumini wake ili ajenge jingo la kisasa la kanisa lake ambalo mwenyewe alisema litakuwa ni la karne. Ni katika kipindi hicho ambapo ujenzi wakanisa hilo ulipoanza ndipo mauaji ya Gleese na mkewe yalipotokea. Polisi wa upelelezi waliona ni vyema wakaanza upelelezi wao kwa kuangalia vyanzo vyake vya mapato pamoja na matumizi.
ITAENDELEA KESHO................

Friday, March 23, 2012

ASPIRINI INAWEZA KUZUIA SARATANI


Vidonge vya Asprin
Kumeza kidonge cha aspirini kila siku inaweza kuzuia na hata kutibu saratani. Taraifa hii ni kwa mujibu wa utafiti mpya.
Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa na jarida la matibabu la The Lancet, na hivyo kuzidisha kuonyesha manufaa ya aspirini katika matibabu ya saratani.
Watu wengi tayari wanatumia Aspirini kama dawa ya maradhi ya moyo.
Lakini wataalamu wanaonya kuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuelezea watu kutumia aspirin ili kuzuia saratani na hata vifo vinavyotokana na saratani.
Wataalamu hao wanaonya kuwa dawa hiyo inaweza kusababisha athari kubwa kama kuvuja damu tumboni.
Prof Peter Rothwell,wa chuo kikuu cha Oxford akiwa na wakufunzi wengine ambao wamefanya utafiti wa hivi karibuni, tayari walikuwa wamehusisha aspirin na kuzuia aina ya saratani hasa saratani ya matumbo.
Lakini utafiti wao wa awali, ulipendekeza kuwa watu wanahitaji kutumia dawa hiyo kwa takriban miaka 10 ili iweze kufanya kazi hiyo.
Sasa wataalamu wanaamini kuwa uwezo wa dawa hiyo kuzuia saratani, hutokea mapema mno kati ya miaka mitatu na mitano. Hii ni kwa mujibu wa taarifa mpya kutoka kwa majaribio 51 yaliyohusisha wagonjwa 77,000.
Na asprini haionekani tu kuzuia tisho la kuugua aina nyingi ya saratani bali pia lakini pia inazuia saratani kusambaa kwa sehemu zingine mwilini.
Hata hivyo majaribio hayo hayakufananisha dawa ya aspirini na dawa zengine zinazoweza kuzuia maradhi ya moyo.
Lakini wakati kikundi cha wataalamu, kilichoongozwa na Profesa Rothwel kilidurusu wangapi kati ya watu waliohusika katika utafiti huo walipata kuugua saratani na hata kufariki kutokana na ugonjwa huo, waligundua kuwa vifo vilitokana pia na matumizi ya aspirin.
Kuzuia kusambaa kwa Saratani
Kwa mtu anayetumia kiwango kidogo cha dawa hiyo kila siku, ilionekana kupunguza idadi ya visa vya saratani kwa robo baada ya miaka mitatu pekee.
Ni watu tisa waliogungulika kuwa na saratani katika watu elfu moja kila mwaka ikilinganishwa na watu kumi na mbili kwa watu elfu moja kwa wale waliomeza tembe hizo.
Pia ilipunguza idadi ya vifo vilivyookana na saratani kwa asilimia kumi na tano.
source:BBC

Thursday, March 8, 2012

MGOMO WA MADAKTARI WAANZA TENA

Wednesday, March 7, 2012

YAWAJE MTU ASIONWE WAKATI YUPO?



Kwa kawaida huwa tunajidanganya na kudhani tunajua mengi sana kuhusu maisha au yote kuhusu maisha, wakati ukweli ni kwamba tunayoyajua ni yale kidogo tu ambayo tumekutana nayo au kujifunza maishani. Mara nyingi mtu anapozungumzia nguvu fulani zilizoko kwenye dunia hii au ulimwenguni anaweza kuonekana kituko.

Hebu soma habari hii ya kweli ambayo imewahi kuandikwa kwenye vyombo mbali mbali vya habari huko Ulaya siku za nyuma.

Peter wa Gloucestershire huko Uingereza alipatwa na jambo lenye kushangaza sana mwaka 1987. Akiwa katikati ya sherehe ya jamaa yake mmoja alishikwa na haja ndogo.
Aliamua kwenda kujisaidia maliwatoni. Nyuma yake kulikuwa na mwanamke aliyekuwa anelekea huko huko maliwatoni {kumbuka sherehe ilikuwa nyumbani ambapo vyoo havikutengwa vya wanawake na wanaume}

Peter alijisaidia haraka na kutoka ili huyo bibie naye akajisaidie. Alimsalimia wakati anatoka chooni baada ya kujisaidia, lakini yule mwanamke hakuitikia. Kwa Peter halikuwa ni jambo la maana sana na hakulitilia manani. Alienda zake sebuleni ambako muziki na vinywaji vilikuwa vikiendelea. Alipofika hapo alienda kukaa kwenye meza ambapo rafiki zake walikuwepo.

Alipokaa alichukua kinywaji chake na kuanza kuzungumza na hao rafiki zake. Lakini hao rafiki zake walionekana kumpuuzia. Kila aliposema wao hawakumjibu wala kumtazama, waliendelea tu na mazungumzo yao. Peter alijua wameamua kumfanyia mzaha, hivyo aliamua kunyamaza ili kujua lengo la ule mzaha wao.

Kwa kuwa alikuwa ameshikwa na hamu ya sigara, aliamua kuinuka na kumfuata bibi yake ili ampatie moto awashe sigara yake. Ajabu ni kwamba, alipofika pale kwa bibi yake na kumnyooshea mkono ili ampatie sigara aliyokuwa anavuta ili awashe yake, bibi yake hakuonekana kujali. Peter alinyoosha mkono karibu na bibi yake huyo, lakini bibie aliendelea kucheza bila dalili kwamba mbele yake alikuwa akiona mtu.

Peter kuona hivyo alikasirika. Ni mzaha gani wakijinga, aliwaza!Rafiki zake pale mezani wamempuuzia na bibi yake tena anampuuzia, kwa nini? Aliamua kurudi chooni ili ajikague vema, huenda kuna kitu hawataki kumwambia kwamba amechemsha, hasa mavazi.

Peter anasimulia: Nikarudi chooni, kufika namkuta yule mwanamke bado anasubiri pale mlangoni labda akiamini kwamba, labda sijatoka humo. Nilipomuona bado anasubiri, nilikumbuka kwamba, nilipotoka nilimsalimu na hakuitikia. 'Yule mwanamke aligeuka na kuniona. Aliponiona alishtuka sana, 'kumbe umeshatoka wala sikukuona, ningejikojolea nikiwa hapa hapa, 'yule mwanamke alisema kwa mshangao'

Peter alisema alipoenda tena sebuleni rafiki zake na bibi yake walimuuliza alipokuwa muda wote huo. 'chooni ndio ukae mwaka mzima?' Walimwambia.
Anasema, alipowauliza kama ni kweli hawakumwona, walimwambia, hawakumwona. Aliwaeleza kilichotokea na wakabaki wameshangaa.

Je wewe imeshakutokea hali kama hiyo? Kama bado au kama hujawahi kuisikia , haina maana kama haipo. Hiyo ni hali yenye kuwatokea watu kwa idadi ya kutosha. Tofauti iko kwenye kiwango tu. Wengine huwatokea kwa muda mfupi sana, kama sekunde tano au kumi na wengine hata dakika tano au zaidi, kama ilivyotokea kwa Peter.

Ni hali ambayo mtu anapoteza uwezo wake wa kuonwa na wengine. Mtu anaamini kwamba wengine wanamuona kama kawaida, wakati wala hawamuoni. Hawamuoni mwili na wala hawasikii sauti yake. Hali hii ambayo kitaalamu hufahamika kama invisibility, huwatokea wengi pengine hata ukiwemo wewe, bali inakuwa vigumu kung'amua kwa sababu unaweza kutafsiri kama dharau.

Kwa mfano, kuna siku nilikuwa ninampa kondakta wa basi la daladala nauli, nikaona hapokei, bali anapokea za wengine tu. Kuona hivyo nilikasirika sana, na kuacha kumpa. Nilishuka kituo kinachofuata nikiwa nimenyoosha mkono ili achukue pesa zake, lakionoi wala hakunitazama, alikuwa anawadai wengine tu.

Kwa sababu naijua hii hali ya invisibility, sikushangaa sana, nilitabasamu. Kwa asiyeijua ataitafsiri kwa njia mbali mbali na hivyo hatajua ukweli.
Kuna wakati mtu anakwenda hotelini, halafu anakuta wahudumu wote wanampita tu , hadi baada ya dakika fulani, kama vile wahudumu wanatoka usingizini ndio wanamwona na kumfuata. Mwingine anaweza hata kufoka, lakini wahudumu wanaonekana hawamjali , kumbe hawamwoni.

Hivi ni kitu gani kinatokea hadi mtu haonekani? Hilo ni swali ambalo bado halijapatiwa jibu. Lakini, huenda Wajapani watatoa jibu hivi karibuni, kwani wamegundua tayari.

NI NGUVU ZINAZO ONGOZA MAISHA

 

Mimi ni muumini wa nguvu za kimaumbile. Naamini kwamba kila kinachopandwa, hatimaye huvunwa kwa njia ile ile, kama leo hii mtu akitenda wema, ni wazi atavuna wema huo, iwe anataka au hataki. Kwa kawaida maisha yetu yanazingirwa na nguvu tunazopanda wenyewe ingawa hili limekuwa gumu kwetu kueleweka.

Naomba nikupe mfano wa watu ambao huenda unaweza kuwafahamu. Miaka mingi iliyopita, mkulima mmoja kule Uskochi, alikuwa akifanya kazi zake shambani. Ghafla alisikia kelele kutoka bondeni .

Mkulima huyo, bwana Fleming alikimbilia huko bondeni kuona kulikoni. Kufika huko, alikuta kuna kijana mmoja ambaye alikuwa anazama kwenye tope.

Kumbuka kwa wenzetu, kuna maeneo ambayo mtu anaweza kukanyaga na kujikuta akizama pole pole hadi kumezwa kabisa na tope na kufa. Mkulima huyu alijitahidi hadi akamwokoa kijana huyo.

Kwa kawaida wakulia wengi hawakuwa tayari kuhatarisha maisha yao, kuokoa mtu ambaye anazama. Kwanza, hadi mtu kufikia mtu kuzama shambani kwako maana yake ni kuwa aliingia eneo lako bila idhini. Lakini, kumwokoa mtu ingekuwa ni sawa na mtu anayeokoa kujiweka katika hatari ya kufa pia. Lakini mkulima huyu alijali zaidi utu wa yule aliyekuwa anaomba msaada.

Kesho yake asubuhi, mkulima yule alishangaa kuona mkokoteni wa farasi umefika nyumbani kwake. Mikokoteni hii ilikuwa ikimilikiwa na watu wenye uwezo au kutoka koo ya kifalme. Mgeni huyu alikuwa ameongozana na yule kijana aliyeokolewa. Mtu aliyekuwa na mkokoteni ule, ambao kwa sasa tungesema Benz ile, alijitambulisha.

Huyu alikuwa ni baba wa yule kijana aliyeokolewa na mkulima yule. Huyu mgeni aliuliza, 'wewe ndiye ndiye uliyemwokoa mwanangu jana? Ninashukuru sana kwa hilo. Nimekuja kukulipa kwa wema wako.' Mkulima Fleming alisema kwamba, hahitaji kulipwa chochote kwa kile alichofanya.

Wakati huo mtoto wa mkulima yule ambaye alikuwa makamu mamoja na kijana aliyeokolewa, alijitokeza kutoka ndani. Yule mgeni aliuliza, 'Huyu ni mwanao,' Yule mkulima alijibu kwa kujidai, akisema, 'ndiyo.' Yule mgeni alisema, 'naomba nimsomeshe kwa kadiri ambavyo ningemsomesha mwanangu.'

Halafu aliendelea, 'Kama ni mtoto ambaye atakuwa na moyo kama wa baba yake, basi atasaidia watu wengi sana na atafanya dunia kuwa mahali bora zaidi.' Mkulima alikubali ofa ile ya mwanae kusomeshwa. Kwa hiyo, kijana akawa amepata mfadhili mwenye fedha kumsomesha kutokana na wema wa baba yake.

Ni kweli, mgeni alimsomesha kijana huyu hadi kiwango cha juu kabisa cha elimu, kwenye shule bora kabisa za wakati ule. Kijana huyu alikuja kusomea udaktari kwenye chuo ambacho kilifahamika kama, St. Mary' Hospital Medical School, kilichopo London, Uingereza. Maana yake ni kwamba alikuwa ni Daktari.

Huyu kijana ni mtu maarufu sana hapa Duniani. Kwa nini? Ni kwa sababu, ndiye mtu aliyegundua dawa aina ya Penicillin. Huyu si mwingine, bali ni Sir Alexander Fleming.

Baada ta kumaliza masomo yake na kugundua dawa hiyo, kilitokea kisa kingine. Yule kijana aliyeokolewa kuzama topeni na yule mkulima, alipatwa na maradhi ya homa ya mapafu {Pneumonia}. Kilichookoa maisha yake kilikuwa ni dawa ya Penicillin ambayo iligunduliwa na mtu aliyesomeshwa na baba yake, katika kulipa shukrani ya msaada uliotolewa kwa mwanae.

Naomba nikwambie kwamba yule Tajiri hakuwa mwingine bali Lord Randolph Churchill, ambaye ni baba wa mtu aliyekuja kuwa maarufu sana duniani kwa uongozi na hekima yake, Sir Winston Churchill. Huyu bwana ndiye aliyeokolewa kule kwenye tope na kuja kuokolewa tena na Penicillin. Umeelewa?

Je, wakati mkulima yule anamwokoa kijana yule, bila masharti au kinyongo, alikuwa anategemea kupata kitu gani kutoka kwake au kwa baba yake, ambaye wala hakuwa akimjua? Hakuwa anategema chochote, bali alitenda wema tu. Tunapotenda wema huwa hatutarajii kulipwa.

Lakini tunapotenda wema, ni kwa namna gani tunaingia kwenye mfumo wa nguvu za kimaumbile? Naomba nitumie habari hii kukufahamisha. Kila jambo jema au baya tunalotenda linatuweka mahali ambapo tunaingia kwenye njia ya nguvu inayoendesha mambo ulimwenguni. Hatuna haja ya kuhangaika kujua, tumeingia katika nguvu gani, kwani tujue au tusijue, tutaingia tu.

Kwa mfano mkulima alimwokoa kijana, badala ya kusema , 'ngoja life, kwa nini hayasikii yakiambiwa yasiingie kwenye maeneo ya watu?' Kumwokoa kwake kulifanya baba wa kijana huyu kutaka kulipa fadhila. Mkulima alikataa malipo mengine yote, bali 'ofa' ya mwanae kusomeshwa . Kumbuka , mkulima kwa njaa yake angekubali hela haraka sana, lakini alikataa.

Kwa kukataa kuuza ule wema aliotenda kwa kijana akawa ameingia kwenye nguvu chanya zaidi. Kukataa huko kulizua tajiri kutaka kumsomesha mwanaye. Kama angekubali fedha, huenda mwanae asingekuja kusoma na kuwa daktari maarufu duniani na mgunduzi wa dawa iliyookoa maisha ya mamilioni ya watu.

Huyu tajiri, naye ameamua kulipa fadhila ambayo ni nguvu chanya. Pale mkulima alipokataa kupokea zawadi ya fedha, yule tajiri bado aliona atajisikia vizuri kumtendea jema mkulima. Alimwona kijana wake na akaona kumsomesha katika kiwango cha juu lingekuwa jambo ambalo lingempa ridhiko. Alifanya hivyo, na hiyo fadhila yake, ndiyo ambayo inakuja tena baadae kumwokoa mwanae.


Habari hii iliwahi kuandikwa katika Gazeti la Jitambue........

Sunday, March 4, 2012

BINTI WA MIAKA 10 AJIFUNGUA MTOTO WA KIUME

Image of Binti wa miaka 10 ajifungua mtoto wa kiume
Binti wa miaka 10 ajifungua mtoto wa kiume


Mtoto huyo, alizaliwa kwa kupitia upasuaji inayojulikana kama Caesarian Section katika Hospitali ya Wanawake katika mji wa Puebla na sasa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa pneumonia.

Msichana huyo anaendelea vizuri kiafya na amesharejea nyumbani baada ya kujifungua, na anamtembelea mtoto wake hospitali kila siku.

Mwendesha mashtaka wa mji wa Puebla anafanya uchunguzi kumtafuta mwanaume aliyefanya ngono na msichana huyo, sababu hiyo inachukuliwa kama ni ubakaji kutokana na umri wa binti huyo.

Hii si maraya kwanza kwa msichana mwenye umri mdogo sana kujifungua nchini Mexico.

Mwezi Agosti mwaka jana, msichana Amalia, aliyekuwa na umri wa miaka 11, alijifungua mtoto baada ya vyombo vya sheria kutomruhusu kutoa mimba (abortion) kutokana na sheria ya Mexico kutoruhusu utoaji mimba ikivuka miezi mitatu.

Amalia alipata mimba baada ya kubakwa mara kwa mara na baba yake wa kambo kuanzia wakati ana umri wa miaka 10.

HOUSEGIRL AWEKA DAMU KWENYE UJI WA MTOTO

Image of Housegirl mwenye HIV achakachua uji wa mtoto wa bosi na damu yake ya hedhi (period)
Housegirl mwenye HIV achakachua uji wa mtoto wa bosi na damu yake ya hedhi (period)Housegirl mwenye umri wa miaka 17 amebambwa akiweka damu yake ya hedhi (period) kwenye uji wa mtoto wa muajiri wake, mwenye umri wa miaka 4. Msichana huyo anayeitwa Pelagia Mureya, alifanya kioja hicho cha kutisha nchini Zimbabwe
kwa mujibu wa website ya NewsDay, Miss Mureya, ambaye ni HIV positive, alifanya kitendo hicho cha kikatili mara kadhaa kabla ya kukamatwa

Uchakachuaji huo uligundulika pale mwajiri wake aliona tone la damu wakati mtoto wake akila uji, na kufanya "uchunguzi."

Baada ya kukamatwa, Mureya alidai hafahamu damu imetoka wapi

Mwajiri wake alichukua uji, mtoto wake na mjakazi Hospitali Gutu Vijijini ambapo vipimo vilithibitisha ilikuwa ni damu ya hedhi ya Mureya.

Mureya, ambaye ni kutoka kijiji cha Chinhoyi, alihukumiwa miaka 10 jela.

Hakukuwa na maelezo yaliyotolewa ni kwa nini aliweka damu kwenye uji wa mtoto wa muajiri wake.

Saturday, March 3, 2012

REMEMBER MICHAEL

http://www.africapoint.net/wp-content/uploads/2009/06/michaelj.jpg
JE, ulikuwa na umri wa miaka mingapi wakati mfalme wa muziki wa Pop wa Marekani, hayati Michael Jackson alipoitembelea Tanzania mwaka 1992 na kufika shule maalum ya watoto yatima na wenye mtindio wa ubongo iliyopo Sinza?
Mwanamuziki huyo aliyekuwa maarufu zaidi duniani hadi anakufa 2009, alifika nchini akiwa balozi wa ziara ya Umoja wa Mataifa na akapokelewa kiserikali na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, hayati Hassan Diria.
Michael Jackson alitua jioni moja uwanja wa ndege wa Dar akiwa amevalia shati la kijani lenye mikono mirefu, suruali nyeusi na kofia nyeusi, akapandishwa kwenye Mercedes iliyompeleka hadi Kilimanjaro Hotel (wakati huo) ambayo baadaye ikawa Kilimanjaro Hotel Kempinsk, sasa ikiitwa Hyatt Regency Dar es Salaam.
http://www.zenjydar.co.uk/2009months/200906/images/michael+jackson+diria.jpgMashabiki waliokuwa na habari walijazana uwanja wa ndege Dar  “kumkodolea mimacho” mwanamuziki huyo wakati huo akiwa na umri wa miaka 34 tu, mbali na wale waliomfuata hadi kwenye hoteli hiyo. Wakaungana na wale waliokuwa wakimsubiri hapo kumshangilia kwa mbinja na mayowe ya furaha.
Pia, mashabiki waliokuwa na habari za ujio na ratiba yake, walijitokeza kwa wingi na kumshangaa vilivyo, The Wacko Jacko alipotembelea shule hiyo ya Sinza, kesho yake.
Katika ziara yake hiyo ya siku mbili nchini, alikutana na mkuu wa nchi ambaye wakati huo alikuwa Rais Ali Hassan Mwinyi.
Ndivyo Michael Joseph Jackson alivyofika Tanzania na kushikana mikono na watoto wa Sinza miaka karibu 20 iliyopita!

BINTI MDOGO AGOMBEA MWANAUME

Binti ambaye umri wake unakadiriwa kuwa kati ya miaka 15-16, aliyefahamika kwa jina moja la Fatuma, amezua sekeseke la aina yake akidaiwa kugombea mwanaume.
Tukio hilo la aibu na kusikitisha lilitokea Februari 29, mwaka huu, saa nane mchana ndani ya Ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni jijini Dar.
Awali, Fatuma alionekana akiwa ameketi na mashosti zake wakipata ofa ya pombe kutoka kwa mwanaume aliyetajwa kwa jina moja la Peter ambapo baada ya muda alitokea demu mwingine na kwenda kukaa meza nyingine.
Ilidaiwa kuwa, yule msichana aliyetinga ukumbini pale alikuwa ni mpenzi wa Peter hivyo katika kuua soo, mwanaume huyo alimtuma mhudumu awapelekee fedha Fatuma na wenzake na kumtaka akawaambie wasimfuatefuate tena.
Baada ya Fatuma ambaye muda mwingi alikuwa akijua kuwa ndiye atakayeondoka na Peter kwa madai ni mzuri kuliko wenzake kuhisi anataka kuachwa solemba, alinyanyuka na kwenda kumletea ‘vagi’ yule demu aliyewatibulia.
Aidha, kibinti hicho kilimporomoshea matusi mazito Peter akimwambia eti anashobokea mademu wenye mititi makubwa wakati kigoli (yeye) yupo.
“Wewe nilikuona mjanja kumbe hauna lolote, mjinga na fala mkubwa wewe,” alisikika akibwatuka binti huyo.
Maneno hayo yaliamsha hasira kwa Peter ambaye alinyanyuka na kuanza kumshushia kipigo Fatuma kiasi cha kuzua timbwili zito na kujaza watu.
Hata hivyo, baadhi ya wasamaria wema waliokuwa eneo hilo waliingilia kati na kumuokoa binti huyo akiwa nyang’anyang’a kwa kipigo.
Akizungumza na gazeti hili nje ya ukumbi huo, binti huyo alisema: “Mimi namshangaa sana yule kaka, kunipiga bila sababu za msingi, kama ni ofa sijamuomba, amenipa mwenyewe, kwa nini anipige?” alihoji Fatuma huku akiondoka eneo hilo akiwa amenyong’onyea.
Mtumishi wa MUNGU mmoja akiwa kwenye gari alisimamishwa na Trafic Police,police
akiwa anahitaji rushwa alianza kuuliza maswali mengi, mara mbona
gari lako linatoa moshi mwingi? mbona gari lako matairi yameisha,
hatimaye polisi akamuamuru padre waende nae kituoni.
Njiani polisi alimuuliza , umesema wewe ni Mtumishi wa MUNGU, je unabiblia
ndani ya gari, akajibu ndio ninayo, polisi akamuambi...a ,
pack gari pembeni na unipe biblia. Mtumishi akapaki gari na kumpa biblia
yule polisi,Polisi akasita kupokea, akamwambia Mtumishi 'fungua na usome
Mathayo 5:25-26 "Mtu wa Mungu akasoma ":
"Patana na Mshtaki wako upesi,wakati uwapo pamoja naye njiani: yule mshtaki asijekukupeleka kwa kadhi na kadhi akakupeleka kwa askari,ukatupwa gerezani.
" Amin nakuambia,Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho"
Mtu wa Mungu akampa yaliyo yake kaizari.
Polisi akatabasamu na kusema 'msifanye migumu mioyo yenu".. Enenda kwa amani.

Thursday, March 1, 2012

http://api.ning.com/files/XDvieCk-6HgMCoWy-Xa5snZikZ4tAo3aaMjAvHl7RxRAPZ8eRira22pKg-WzdeZHspdHS18PcUYtO0eS4wtGM3CaNTC6EP*W/theopilkk.jpg

CHADEMA WAMCHAGUA NASSARI ARUMERU


 Joshua Nassari
 
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemchagua Joshua Nassari kupeperusha bendera yake katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, utakaofanyika Aprili Mosi, mwaka huu.

Akitangaza matokeo ya uteuzi huo, Mkurugenzi wa Bunge na Oganaizesheni wa Chadema, John Mrema alisema Nassari ameteuliwa baada ya kupata kura 805 sawa na asilimia 90.6 ya kura zote 888 zilizopigwa.

Alisema Nassari aliwaangusha Anna Mghiwa aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata kura 23, akifuatiwa na Godluv Simba (18), Rebecca Magwisha (12), Samweli Shami (10), Anthony Mussari (8) na Yohanne Kimuto (6).
“Kura zilizopigwa zilikuwa 888 zilizoharibika ni sita na wagombea wote wametangaza kukubali matokeo,” alisema Mrema. Msimamizi wa uchaguzi huo alikuwa ni mwasisi wa chama hicho, Edwin Mtei.
Ukumbini

Mgombea Musari aliyehamia Chadema baada ya kuangushwa kwenye mchakato wa kutafuta mgombea kupitia CCM aliwaambia wajumbe kwamba, tayari alikwishafukuzwa kazi ya ukuu wa shule hivyo aliomba wajumbe wampigie kura kupeperusha bendera ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini katika uchaguzi huo.

Kauli ya mgombea huyo ilimfanya mmoja wa wajumbe kutoka kata ya Maji ya Chai kumhoji iwapo hatahama tena Chadema akikosa kura katika uchaguzi huo wa jana, naye akaahidi kushirikiana na wana Chadema wenzake kutafuta ushindi wa chama chake hicho.

Awali, mzee Mtei alisema chama hicho kinahitaji wabunge wenye kuendesha na kutekeleza sera zinazojibu mahitaji ya
wananchi na jamii wanayoongoza kwa kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote bila kujali tofauti miongoni mwao.

“Hivi sasa wananchi wengi wanakula mlo mmoja kwa siku sababu hawawezi kumudu gharama ya milo miwili na hili linasababishwa na usimamizi na uongozi mbovu wa Serikali ya CCM,” alisema Mtei.

Aliwaasa wana Arumeru kupuuza rushwa inayodaiwa kuwa imeanza kusambazwa sehemu mbalimbali za jimbo hilo na wanaodaiwa kuwa viongozi au wanachama wa CCM na kuchagua kiongozi wanayeamini kuwa atawakilisha hoja na fikra zao bungeni bila kushaiwishiwa kwa rushwa.

CCM wakamatwa kwa rushwa
Katika hatua nyingine, viongozi watatu wa CCM, wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kuhusiana na kura za maoni za marudio ndani ya chama hicho.
Kura za maoni zinatarajiwa kupigwa leo na wagombea wawili
walioongoza katika awamu ya kwanza ya kura za maoni zilizofanyika wiki iliyopita, Siyoi Sumari na Wililiam Sarakikya watapigiwa kura.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Mbengwa Kasomambuto alithibitisha jana kwa simu kushikiliwa kwa viongozi hao ambao hata hivyo, alikataa kuwataja majina kwa sababu ya kiuchunguzi.

“Kweli tunawashikilia wana CCM watatu kwa mahojiano baada ya vijana wangu waliotapakaa kila sehemu ya Jimbo la Arumeru Mashariki kuwakuta katika mazingira yanayoashiria uwepo wa rushwa,” alisema...Soma zaidi www.mwananchi.co.tz