Wednesday, February 29, 2012

ZITTO AKANUSHA KUGOMBEA URAIS 2015




KABWE ZUBERI ZITTO, MP
KIGOMA KASKAZINI


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Kampeni ya kupunguza umri wa urais haina uhusiano na mimi kutaka kugombea urais 2015

1. Baadhi ya vyombo vya habari vimehusisha kauli yangu ya kutaka kupunguza umri wa kugombea urais na mimi ‘kuutaka urais’. Mimi nikiwa mwanachama na kiongozi wa chama chama changu cha CHADEMA naelewa na kuziheshimu taratibu na kanuni tulizojiwekea za kuomba nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo nafasi ya urais. Nafasi ya uongozi ndani ya CHADEMA haiombwi kwenye warsha. Iwapo chama change, wakati muafaka ukifika na kutokana na matakwa ya jamii, kikiona nipewe jukumu lolote sitasita kutekeleza wajibu huo niwe au nisiwe mgombea.

2. Kwa hivyo, nilichozungumza jana ni kutoa maoni yangu kwamba muda umefika kwa Taifa letu kupunguza umri wa kugombea urais. Maoni yangu haya yanatokana na ukweli kwamba hakuna sababu zozote za kisayansi zinazomfanya mtu aliye chini ya umri wa miaka 40 akose sifa za kuwa Rais. Msimamo huu nimekuwa nao tangu zamani nikisoma shule na haujawahi kubadilika. Hakuna mahala popote katika maoni yangu niliyotoa jana niliposema kwamba nataka umri wa urais upunguzwe ili nipate fursa ya kugombea nafasi ya urais. Pia siwezi kutaka katiba iandikwe kwa ajili yangu. Vilevile kamwe isionekane kwamba matakwa ya muda mrefu ya vijana ya kutaka umri wa kugombea Urais kupunguzwa yanalenga kunipa fursa mimi kwani mimi ni binaadamu naweza nisiwe na sifa za kuwa Rais lakini kukawa na vijana wengine wengi wenye umri chini ya miaka 40 wenye Uwezo na Uzalendo wa kutosha kushika usukani wa nchi yetu. Ni maoni yangu kwamba tupate mabadiliko ya vizazi katika uongozi wa nchi yetu ili kukabili changamoto za sasa zinazokabili Taifa letu.

3. Tunapojiandaa kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya ni vizuri vyombo vya habari vikajikita kutoa taarifa bila kuweka tafsiri au kuwatafasiria maoni ambayo wananchi na viongozi watakuwa wanayatoa kuhusu maudhui ya Katiba Mpya.

HATARI

Mwanamke alinunua line mpya ya voda ili ampime mumewe.Wakiwa wameketi sebuleni,mwanamke alienda jikoni na kumpigia mumewe,huku amebadilisha sauti.Jamaa akapokea simu"Hallow"
WIFE:Hallo darling wangu naona siku hizi umenisusa
JAMAA:Pliz,Kata nitakupigia
Ghafla jamaa akatoka nje kibarazani,na kumpigia darling nae akapokea
WIFE: Hey swity,mbona umeniambia nikate simu?uko wapi?
JAMAA:Niko home.Lile ling'ombe lilikua jikoni, lingenikuta naongea na wewe ingekua noma

CHADEMA NA CCM KAMA REPUBLICAN NA DEMOCRATC



Inavyoanza kuonekana kwa sasa vyama hivi pekee ndivyo vitakuwa vikimenyana kwenye chaguzi kubwa.ni kama marekani.Naambiwa kule japo kuna vyama vingi sana vidogo hata vya kikomunisti,lakini nyote mnajua kuwa kwa karne sasa ni Republicans na Democrats pekee wanaotawala hasa siasa za nchi hiyo.Mwenendo ulivyo kwa sasa hapa nchini Ni CHADEMA na CCM. Tangu uchaguzi wa 2005 dalili hizi zilianza kuonekana hasa bungeni ambapo ungedhani kulikuwa na wabunge wa vyama hivyo pekee.japo CUF kiliongoza upinzani bungeni lakini kwa maoni yangu ni wabunge wa CHADEMA wale 11 waliojenga taswira ya upinzani.uchaguzi wa 2010 umeiweka CHADEMA kuwa Kambi rasmi ya upinzani pamoja na sarakasi za Hamad Rashid na Kafulila ambazo zilishindwa.
Mnaokumbuka tena katika chaguzi zote ndogo tangia 2005, ni CHADEMA na CCM ndo vimekuwa na ushindani wa kweli.Mnakumbuka kiteto,Tarime,Biharamulo,Busanda,Mbeya Vijijini,Igunga,Uzini,na sasa Arumeru? baadhi ya vyama vimekosa hata pumzi ya kuingia kwenye uchaguzi.
Kwa hiyo hakuna haja ya kuunganisha vyama vya upinzani kama ilivyokuwa inasemwa na baadhi ya watu hata wasomi.vyama vinaweza kuungana mkono tu na siyo kuungana.vilevile hakuna haja ya kuogopa kusajili vyama vipya kwani hata vikiwa 1000 itabaki kuwa CHADEMA Vs CCM.Kweli tunakoelekea ni kuzuri
Mdau

KWA NINI WASICHANA HUBABAIKIA WENYE MAGARI NA FEDHA?


Inasemekana wasichana wa mijini wanadanganyika zaidi kwa magari. Msichana anakubali kuwa na uhusianao na mwanume kwa sababu amegundua kwamba ana gari, hata kama anajua kwamba hilo gari sio la huyo mwanaume, lakini hujikuta akikubali kuwa na uhusiano na mwanaume huyo kwa sababu ya gari tu.

Ndio maana madereva wengi hasa wale wa teksi wanajisifu kwamba wanawake wanawapapatikia sana.

Je hili lina ukweli kiasi gani?

Lakini je ni wasichana wote ambao wanawapapatikia madereve au watu wenye magari?
Nadhani hili ndilo swali gumu sana kwenye suala hili
Kila kitu kinachohusu uhusianao wa kimapenzi, tunajifunza kutoka kwa wazazi au walezi wetu, labda asilimia 10 tu ndio tunayojifunza nje ya nyumbani.

Siyo suala la gari peke yake, bali ni suala la karibu kila kitu. Je watoto wetu tunawajengea dhana gani kuhusu kila kitu kwenye maisha?
Halafu tunawaambia kitu gani kuhusu kupenda?
Siku zote na tulio wengi tunawaambia watoto wetu uongo mwingi sana, na uongo huo unatokana na sababu nyingi.
Kwanza nasi tulidanganywa na wazazi wetu. Pili hatujiamini. Tatu hatuna uhakika sisi ni akina nani, na nne tunadhani uongo huo utawasaidia watoto wetu.
Hebu chunguza kwa makini utagundua kwamba, wasichana wanaobabaikia magari ni wale ambao wamelelewa kwenye malezi ya uongo mtupu.

Unaweza kudhani wale waliotoka kwenye familia masikini ndiyo ambao wanababaikia magari, hapana.
Msichana anaweza kutoka kwenye familia masikini na asibabaikie utajiri wala magari, wako wengi wa aina hiyo.
Kama nyumbani wazazi wanawasifu wenye magari, wanaonesha kwamba ukiwa na gari ndio unakuwa na maana, kwamba ndio kiwango cha juu cha mafanikio, unatarajia kitu gani kutoka kwa watoto?
Kuna wakati wazazi wanasema , “ameshafika mbali sio mwenzio, yule ana akili sana. Ana magari mawili na nyumba tatu.

Wakati mwingine inatosha mara moja tu, jambo kusemwa na mzazi, na mtoto kuamini kwamba mwenye gari au magari na nyumba ndiye aliyekamilika, ndiye mwenye akili..

Kumbuka mtoto anaingiza maarifa akilini mwake kutoka kwa watu anaowaamini anaokutana nao maishani. Kwenye suala la uhusianao wazazi ndio wanaoaminika zaidi.

Kwa sababu ya umasikini wetu, tulio wengi na uhaba wa malengo makubwa kuliko sisi wenyewe, gari na nyumba ndio malengo ya juu kabisa ya binadamu kuyapata.

Mtoto anakuwa na akili ya aina hiyo, kigezo chake kuhusiana na mtu kitakuwa ni gari, nyumba au mali kwa ujumla.
Kwake binadamu mwenye maana na anayefaa ni yule anayemudu kumiliki vitu hivyo.

Hii sio kwa wasichana peke yake bali hata wanaume. Kama mtoto wa kiume alioneshwa kuwa thamani ya mtu inatoka kwenye gari, nyumba na mali, basi naye atakuwa anababaikia vitu hivyo.

Linapokuja swala la uhusianao, atajitahidi kumuonesha msichana kwamba anavyo vitu hivyo au anao uwezo wa kuvimiliki. Anafanya hivyo kwa sababu aliambiwa thamani yake inakuwepo pale anapokuwa na vitu hivyo.

Wazazi wengi wameegemeza thamani zao kwenye vitu badala ya wao wenyewe. Bila ya hiyari yao wanawafundisha watoto wao kujali na kuthamini vitu badala ya utu wao.
Kwa kadiri mfumo wa maisha wa mitaji ulivyokuwa ukiendelea, binadamu alijitoa thamani na kuiweka kwenye vitu, hasa mali.

Kwa bahati mbaya wale watoto wa wazazi ambao wana maisha ya kati ndio ambao wanasumbuliwa na mali.

Kwa nini?

Kwa sababu wazazi wao hawajui kama wako juu au chini kimapato.

Katika kujitafuta hutoa kauli zenye kuonesha kwamba maisha ni mali, basi.

Wazazi walio na kipato cha chini nao wanaweza kuwaathiri vibaya watoto wao, kwa kuzungumza na kutenda katika njia ambayo watoto wataamini kwamba umasikini huondoa kabisa thamani ya mtu.Wale walio juu kabisa wanaweza wasifikirie kwamba gari au nyumba ni mambo ya maana sana, hata kama wamefundishwa kuhusu mali. Wao watafikiria mali kwa mkabala mkubwa zaidi.

Labda watafikiria kuhusu ndege au kutembelea boti ya kifahari na mengine, lakini wote watakuwa na udhaifu ule ule wa kuamini kwamba mali ni kubwa kuliko thamani ya binadamu.
Mali ambayo unaitengeneza na kuitafuta mwenyewe halafu iwe kubwa kuliko wewe! Hii ni ajabu kabisa.

Wazazi ambao wanachukulia mali kama kitu cha kawaida sana, ambacho uwe nacho au usiwe nacho, maana ya maisha haibadiliki, na thamani yako haiondoki kamwe, hawa ndio watoto wao watakuwa na maisha bora.

BALOZI MAHALU AMLIPUA JK MAHAKAMANI





ANIKA ALIVYOSHIRIKI KATIKA MCHAKATO KIPINDI AKIWA WAZIRI MAMBO YA NJE, ASEMA ALIKUTANA NA MAMA MWENYE NYUMBA NA KUAGIZA ALIPWE DOLA MILIONI MOJA HARAKA, AKAMPA OFA KUJA MBUGA YA NGORONGORO
Tausi Ally
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alifahamu kuwepo kwa rasimu mbili za mikataba ya ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania, Italia.

Profesa Mahalu alisema hayo jana mbele ya Hakimu Mfawidhi, Ilvin Mgeta wakati akitoa utetezi wake dhidi ya kesi inayomkabili ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 pamoja na aliyekuwa Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.

Akiongozwa na wakili wake, Mabere Marando, Profesa Mahalu aliitambua barua ya Februari 20, 2002 ambayo ilikuwa ikieleza kuwa matayarisho yote ya ununuzi wa jengo la ubalozi huko Italia yamekamilika ikiwa ni pamoja na rasimu mbili za mikataba.

Mahalu alidai kuwa katika mchakato wa ununuzi wa jengo hilo wakati yeye akiwa Balozi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kulikuwa na rasimu mbili za mikataba na kwamba aliwahi kuwasiliana na wizara hiyo juu ya mikataba hiyo.

Alidai kuwa Desemba 2001, Kikwete wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alikwenda Rome, Italia kwenye Mkutano wa SADC na alipokuwa huko, ubalozi ulifanya mpango atembelee jengo hilo lililopendekezwa kununuliwa kwa ajili ya ofisi ya ubalozi.

“Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia ilifanya mipango yote kwa kumpa utaratibu na usalama Kikwete ambapo alikwenda kutembelea jengo hilo na kukutana na mama mwenye jengo,” alidai Profesa Mahalu.

Alidai kuwa kabla ya mazungumzo na mwenye nyumba, mtoto wa mama huyo, Alberto alimtembeza Kikwete kwenye jengo hilo ndani na nje na baadaye mazungumzo hayo yaliendelea.

Balozi Mahalu alisema baadaye mazungumzo kati ya Kikwete na mama huyo yaliendelea na Alberto alikuwa akitafsiri, kwa sababu mama yake hakufahamu lugha ya Kiingereza.

Profesa Mahalu alidai kuwa katika mazungumzo hayo, Kikwete alimwuliza mama huyo: “Hivi ni kwa nini kunakuwa na mikataba miwili?” na mama huyo alimjibu kuwa hiyo ni kawaida kwa Italia ukitaka kununua jengo kwa bei nafuu.

Profesa Mahalu aliendelea kudai kuwa baada ya kupewa jibu hilo, Kikwete hakuzungumza tena zaidi ya kucheka na kwamba mwenye jengo alimkumbusha kuhusu malipo ya awali ya dola milioni moja za Marekani ambapo aliafiki na kuahidi kuwa zingelipwa kabla ya mwisho wa mwaka 2001.
Profesa Mahalu alidai pia kwamba Kikwete alimweleza mama huyo kuwa atalishughulikia suala hilo baada ya kurejea Dar es Salaam na kumshukuru kwa kuwauzia jengo zuri.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya Kikwete kusema maneno hayo, alimgeukia na kumwambia: “Costa ni vizuri tupate hela tumlipe huyu mama watu wengine wasije wakachukua hili jengo.”

Profesa Mahalu alidai kuwa baada ya Kikwete kumshukuru mama huyo kwa ukarimu wake, alimkaribisha Tanzania awe mgeni wa Wizara ya Mambo ya Nje yeye na mumewe na kwamba watampeleka Ngorongoro.

“Tulipokuwa njiani tukirudi hotelini alipofikia Kikwete akiwa kwenye gari alimpigia simu Kibero akimuagiza afanye utaratibu wa kulipa Dola milioni moja kama malipo ya awali ya jengo hilo,” alidai Profesa Mahalu.

Alidai kuwa baadaye alimwagiza (Profesa Mahalu) aje Dar es Salaam kufuatilia mpango huo wa malipo ya awali ya ununuzi wa jengo hilo.

Awali, Profesa Mahalu akiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa alidai kuwa anaitambua ripoti ya uthamini wa jengo hilo la ubalozi nchini Italia uliofanywa na Kimweri kutoka Wizara ya Ujenzi aliyekwenda Rome Julai 15 hadi 26, 2001 kwamba jengo lilikuwa na gharama ya Sh6 bilioni.

Thursday, February 23, 2012

POLISI WAUA SONGEA

 






Kuna raia wanauawa tangu juzi na matukio yanaripotiwa ila askari hawachukui hatua yeyote ile zaidi wanasema ushahidi hawajauona,usiku wa kuamkia leo limekua tukia la 5 raia kuuliwa na askari kama kawaida yao hawatoi ulinzi kwa raia wao.

Asubuhi raia (Watoto, vijana, wazee) wakaamua kuwatolea uvivu askari na kuandamana hadi kituo cha polisi kudai haki ya kulindwa na kuishi raia walikua wengi kuliko uwezo wa askari wa kile kituo hivyo waliona hapa wakiwa wakali kituo kitachomwa moto maaana walikuja na jazba raia wakawaambia taarifa ziko kwa mkuu wa wilaya raia bila simile wakaanza maandamano hadi kwa mkuu wa wilaya kufika huko naye akanawa mikono kama pilato akasema mkuu wa mkoa ndo liko mikononi mwake.

Raia hawakuishia hapo wakalianzisha hadi kwa mkuu wa mkoa huku wakiimba "TUMECHOKA KUUWAWA" hadi kwa mkuu wa mkoa, hapo ndo movie ilpoanzia kumbe raia wakati wanaenda kwa mkuu wa mkoa inaaminika simu zilipigwa kwa mkuu wa mkoa na askari wanaolinda (FFU) wakafunga geti hapo ndo ikawa vuta nikuvute raia wakaweka kambi nje huku wanaimba nyimbo "MKUU WA MKOA UNAWAOGOPA RAIA WAKO JIUZURU", muda si mrefu gari ya FFU likawasiri likiwa na askari wa kutosha kwa vile raia hawakua na silaha wala ugomvi wakaamua kubaki huku wanaimba.

Askari kama kawaida yao wakawa wanazidi kusogelea huku wakitoa ishara wananchi watawanyike huku wananchi wakigoma hawatoki hadi mkuu wa mkoa naye atoke nje hapo ndo askari wakaanza kufyatua risasi za moto na raia wawili wakafa.habari zikafika mjini raia wameuliwa na askari hapo ndo mji ukazizima raia wakaingia mitaani askari waliokua mitaani walianza kupata upinzani mkali hd askari wawili wamekufa hadi hivi sasa, imebidi jeshi liingilie kati na mji wote kufungwa hivi ss mjini ni makundi ya wanajeshi na askari ndo yametawala hakuna maduka wala mabenki yanayofanya kazi
 Kutoka Mabadiliko


Wednesday, February 22, 2012

KANISA LENYE IMANI YA KISHETANI LA TAPELI WAUMINI

 

KANISA moja huko Mlandizi, wilayani Bagamoyo, Pwani, limeingia katika kashfa ya kuwatapeli mamilioni ya fedha waumini wake kwa kisingizio cha kuziombea fedha ili kuondoa mikosi kwa kuzifanyia ibada ya utakaso. Uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha kuwa ibada katika kanisa hilo, inafanyika ili kuwaombea watu wenye matatizo ya fedha na magonjwa.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, fedha zinazoletwa kwa ajili ya kuombewa, zinawekwa kwenye sanduku maalumu linaojulikana kuwa ni sanduku la agano na baadaye kuombewa kwa muda kabla kuzirejesha kwa muumini.
Mmoja wa waumini waliodai kuibiwa fedha zao, kwa njia hiyo na ambaye hakutaka jina ake litajwe gazetini, alidai kuwa analidai kanisa Sh20 milioni, alizozitoa kwa nyakati tofauti ili ziombewe.

“Nilimpa mtumishi fedha ili aziombee na kuzifanyia utakaso kwa sababu alisema mara nyingi fedha tunazotumia zina mashetani,” alisema muumini huyo ambaye ni mwanamke.

“Unajua kuna wakati mtu unafanya biashara lakini, haitoki, hupati faida, sasa watumishi wa Mungu wanasema kunakuwa na mikosi kama vile chuma ulete. Ndiyo maana nilimkabidhi aziombee,” alisema.
“Mara ya kwanza nilipojiunga nilitoa Sh 600,000 ambazo aliziombea na baada ya miezi minne alinirudishia. Mara ya pili nilikuwa nasafirisha mzigo wa thamani ya Sh 7.5 milioni kwenda Zimbabwe. Siku hiyo walikuja dukani kwangu Kariakoo na kuniambia kuwa itabidi nitoe fungu la kumi la mzigo huo yaani Sh750,000 ambazo hata hivyo, walisema watanirudishia,” alisema.

“Kwa kuwa sikuwa na fedha hizo nililazimika kukopa nikijua kuwa watazirudisha kabla sijasafiri. Kesho yake nilipozifuatilia Mlandizi nikakuta wamesafiri kwenda Moshi, ila wameniachia Sh 75,000 wakisema hilo ndiyo fungu la 10 langu.”

Alisema kiongozi huyo wa kanisa na wenzake walimpa masharti ya kutoa ‘chenji’ fedha atakazopata faida isipokuwa nauli, pesa ya kulipa hoteli na ya chakula tu. Alidai kuwa alipotoka Zimbabwe, watumishi hao walimpigia simu wakimtaka akutane nao Makambako, mkoani Iringa kwa madai kuwa Roho Mtakatibu amewaagiza wakafanyie ibada katika mji huo.

Alisema ingawa ya hakuwa na fedha za Kitanzania lakini kwa faida ya Dola 4,800 alizopata kwenye biashara zake, aliwatii na kushukia Makambako.

“Pale Makambako ndiyo nyumbani kwa wazazi wa huyo mtumishi, tulifanya ibada kuanzia saa saba usiku. Wakaniambia nitoe fedha zote nilizonazo ili waziombee. Nikamwambia itabidi azirudishe mapema kwa sababu nilikuwa na order ya kupeleka mzigo nchini Zambia. Akasema atazirudisha mapema,” alidai muumini huyo.

Alidai kuwa walikaa Iringa kwa muda wa siku tatu na kwamba waliporudi Dar es Salaam, mtumishi alianza kumzungusha licha ya kukumbushwa kila mara. “Badala ya kurudisha fedha kama tulivyokubaliana, alinipigia simu akisema twende kwenye maombi Mlandizi saa saba usiku. Huko tena akasema zile fedha itabidi ziombewe kwa siku saba zaidi. Siku saba zilipokwisha bado alisema ameambiwa na Roho Mtakatibu kuwa fedha zikae kwenye Sanduku la Agano kwa siku 21 zaidi,” alidai.

Alidai kuwa wakati wakiendelea kusubiri siku hizo, mtumishi alimshauri asiendelee tena kufanya biashara.
Kwa mujibu wa mtu huyo, pamoja na kuzungushwa lakini bado aliendelea kumwamini mtumishi kiasi cha kumpa fedha nyingine alizotaka.

Alisema kijana mmoja wa Kitanzania anayeishi naye alitaka kufanyiwa maombi ili mambo yake ya mwendee vizuri na kwamba yeye alimshawishi aje kufanyiwa maombi kwenye kanisa hilo.

“Yule kijana akaja kutoka Zimbabwe kwa ajili ya maombi hayo Siku hiyo mtumishi alikuja nyumbani Kinondoni. nikamtambulisha mgeni wangu kwake. Baada ya kusalimiana, alimwita kisha akamuuliza, una fedha hapo mfukoni. kijana akasita kwanza halafu akaja nje kuniuliza, ‘huyo mama anauliza kama nina fedha mfukoni lakini nimeshindwa kumjibu’. Mimi nikamwambia ampe tu” alisema.

Kwa mujibu wa muumini huyo, kijana huyo alikuwa na a Dola 5,900 na Randi 1,000 ambazo zote aliamriwa kumkabidhi mtumishi kwa maelezo kwamba zinakwenda kuombewa na baadaye kurejeshwa.
Taratibu za ibada Habari zimeeleza kuwa ibada katika kanisa hilo inategemea uongozi wa Roho Mtakatifu na hakuna ratiba maalumu.

Mmoja wa wawatumishi wa kanisa hilo (jina tunalo), alisema hakuna ratiba maalumu hadi pale roho wa bwana atakavyowaambia.

“Hii ni huduma ya maombezi ambayo ukija hapa, tunakuuliza mahitaji yako, kisha tunakufanyia maombi. Unajua sisi hatuombi kama makanisa mengine. Tunafuatilia mzizi wa tatizo la mtu tangu kizazi cha kwanza. Kama wewe hukufanya matambiko na maagano, inawezekana wazazi wako au hata babu zako. Hayo yote tunayavunja kwa jina la Yesu. Muda wa maombi utategemea uzito wa tatizo,” alisema Kuhani huyo.

Baadhi ya watu walioko karibu na kanisa hilo, walisema misururu ya magari imekuwa ikufurika ikiwa na watu wanaofanya ibada katika kanisa hilo hasa nyakati za usiku.

“Hapa kila siku wanakuja matajiri na magari yao ili kuombewa na mara nyingi ibada zinafanyika usiku,” alisema mwana kijiji ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini. Siku ya maombi Akisimulia jinsi ibada ya kumwombea kijana huyo ilivyofanyika, mwanamke huyo alisema waliandaa mbuzi, maziwa, pombe ya mbege, mvinyo, vitambaa vya rangi mbalimbali, mtama na ulezi.

“Alisema vitu vyote hivyo ni kwa ajili ya kutengua laana alizowekewa na mababu zake. Ibada ilifanyika usiku wa manane huku yule kijana akiogeshwa kwa mvinyo, uliochanganywa na damu ya mbuzi na sarafu za amani huku akiombewa. Baadaye vile vitu vilichanganywa na biblia mpya na kufukiwa kwenye shimo. Yule kijana alioga na kwenda kupumzika. Hata hivyo, ibada iliendelea kwa siku tatu.” Alisema baadaye kijana aliambiwa asubiri kwa muda wa siku 21 ndipo akachukue fedha zake huku akitakiwa kujitakasa ndani ya siku hizo, lakini hadi sasa hajapata fedah hizo.

Sanduku la agano Kwa mujibu wa mwanamke huyo, baada ya kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Oysterbay na Polisi Mlandizi, alipewa ushirikiano iliowezesha kumkamata huyo mtumishi huku wakifuatilia kilichomo ndani ya Sanduku la Agano. “Siku hiyo tulikwenda na polisi kwenye kanisa hilo usiku, wakalitafuta bila mafanikio. Ikabidi waondoke. Ila wakati tunaondoka nilitumiwa ujumbe mfupi na mmoja wa waumini kuwa limefukiwa karibu na madhabahu.

Alisema siku iliyofuata polisi walilifukua na kulipata na kwamba walipolifungua walikuta bahasha nyingi, msalaba, Biblia, kitabu cha Tenzi za rohoni na fimbo.

Muumini mwingine wa kiume, ambaye pia ni mfanyabiashara naye alidai kutapeliwa Sh1.2 milioni alizoambiwa kuwa ni kwa ajili ya ‘Baraka za Ibrahim’ yaani makabila 12 ya Israel.............

BI.HARUSI ASASWA AKIJIUZA BUGURUNI



Mwanahamisi Hamis akifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Sokoine Drive, Dar es Salaam.

Mwanahamisi Hamis (wa kwanza kushoto) akiwa na wenzake Salima Juma na Halima Amir kizimbani.

Mwanahamisi akitafakari jambo.
Na Richard Bukos
AMA kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni. Usemi huu unakamilishwa na tukio la hivi karibuni ambapo msichana aliyefahamika kwa jina la  Mwanahamisi Hamis, mkazi wa Buguruni, Dar es Salaam na wenzake wawili, Salima Juma na Halima Amir, walipandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi, Sokoine Drive, Dar na kusomewa shitaka la kunaswa sehemu ya wazi wakidaiwa kujiuza.
Wakati kesi ikiendelea, ilibainika kuwa Mwanahamisi ni Bi. Harusi mtarajiwa na vikao vya harusi vilikuwa vikiendelea huku ndoa yake ikitarajiwa kufungwa mwishoni mwa mwezi huu, takribani saa 120 kuanzia leo.
Kwa mujibu wa mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Richard Magodi, mnamo Februari 16, mwaka huu, majira ya saa saba usiku, washitakiwa hao walikamatwa maeneo ya Buguruni wakifanya vitendo haramu vya ukahaba.
Washitakiwa wote walikiri kutenda kosa hilo lakini walimuomba hakimu anayesikiliza kesi yao, Timothy Lyon awasamehe kwa vile ilikuwa mara yao ya kwanza kufikishwa mahakamani hapo kwa kosa hilo.
Pamoja na ombi hilo, mwendesha mashitaka Magodi alimuomba hakimu kutoa adhabu kali kwa washitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine wenye vitendo kama vyao.
Baada ya msumari huo wa mwendesha mashitaka, hakimu aliahirisha kesi hiyo na kuwanyima dhamana washitakiwa mpaka Februari 20 (juzi).
Hata hivyo, Mheshimiwa Lyon alimhukumu mshitakiwa Salima Juma kwenda jela miezi 6 kufuatia kuonesha utovu wa nidhamu mahakamani pale alipomtaka hakimu atengue maamuzi ya awali.
Kifungo hicho kilimfanya Salima kuangua kilio akiwa haamini masikio yake.
Wakati huo huo, watu waliodaiwa kuwa ni miongoni mwa wanakamati wa harusi ya Mwanahamisi walionekana wakihaha mahakamani hapo kumnasua Mwanahamis kwenye aibu baada ya hakimu kuwanyima dhamana.
“Hii sasa aibu jamani, yule Mwanahamisi ni Bi. Harusi mtarajiwa, badala ya kutulia nyumbani anazurura hovyo usiku wa manane mpaka anafedheheka kiasi hiki,” alisema mwanamke mmoja aliyedai ni mwanakamati wa harusi hiyo.
Hata hivyo, mwanamke huyo alifunga ‘bakuli’ lake kufuatia kugundua kwamba alikuwa akihojiwa na paparazi wa gazeti baada ya kujitambulisha kwa ajili ya kupata data zaidi za harusi hiyo...........

MAMA APATIA MIMBA MOCHWARI




Mwanamama mmoja nchini Marekani anayefanya kazi mochuari ameingia matatani baada ya kupata uja uzito kwa kujamiiana na mtu aliyekufa. Mtandao wa habari wa dead serious news umesema tukio hilo linadhaniwa kutokea katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Mourning Glory, nje ya Lexington, Missouri.
Polisi wa mjini humo wamemshtaki mama huyo aitwaye Felicity Marmaduke kwa kosa la kunajisi na kuchezea maiti. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na polisi, kiungo cha kiume cha mwili wa mtu aliyekufa kilihamasika wakati mwili ukioshwa. Taarifa zinasema, kwa kuwa mwanamama huyo alikuwa peke yake, aliamua kujamiiana na mwili huo.
Kwa mshangao hata wa mwanamama huyo, maiti huyo alitoa mbegu za kiume. Wiki chache baadaye Bi Marmaduke alijikuta ni mja mzito. Baada ya kumwambia daktari wake mfululizo wa matukio, daktari huyo aliwataarifu polisi.
Bi Marmaduke alikamatwa na polisi akiwa nyumabni kwake, si mbali sana na mochuari anayofanyia kazi. Katika tukio la kushangaza zaidi, mwanamama huyo amesema anapanga kudai urithi kutoka kwa familia ya mtu huyo aliyekufa......

BAADA YA KUPATANISHWA HIKI NDIO WALICHOSEMA RUGE, SUGU & NCHIMBI!

Waziri wa habari, vijana utamaduni na michezo Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi (MR II), Meneja uzalishaji vipindi Clouds Media Group Ruge Mutahaba & Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu.
Hatimae Waziri wa habari Emmanuel Nchimbi kwa kushirikiana na mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu wamefanikiwa kusuluhisha mgogoro wa kimaslahi kati ya mbunge wa mbeya mjini Joseph Mbilinyi na meneja uzalishaji vipindi CLOUDS MEDIA GROUP Ruge Mutahaba kuhusiana na haki za wasanii wa muziki wa bongofleva.
Waziri Nchimbi amesema “wamekubaliana na kusaini kumaliza tofauti baada ya kufanyika kikao cha mwisho cha upatanishi kati ya Ruge na Mr II ambapo katika upatanishi huo, pande zote mbili ziliridhika kuwa msingi wa mgogoro wao ni kuamini kwamba upande mmoja hauutendei haki upande mwingine”
Waziri Nchimbi amezidi kuamplfy kwamba “kwenye hotuba yangu kwenye bunge lililopita kuhusu vijana Afrika, nilizungumzia haja ya watu kumaliza tofauti zao na kusameheana ambapo baada ya kutoka kwenye mkutano ule Mh Joseph Mbilinyi alikuja kuniona akaniambia muheshimiwa Waziri unajua umeongea mambo ya maana lakini nilitarajia baada ya kusemea pale kwenye kipaza sauti ungekuja kuniambia mimi, haya tuanze huo mchakato wa suluhu, nikamwambia hatujachelewa, bado tunaweza kufanya, nikamuuliza kama ni kweli tufanye mazungumzo ya kuwapatanisha wote wakakubali baada ya kufanya vikao vya kutosha”
Kwa upande wake Ruge Mutahaba amesema “tumepanga mikakati ya jinsi tutakavyokua tunakutana na Mh Sugu kuendelea kusaidia sanaa yetu hii, ni kweli kabisa tumesaini bila shinikizo lolote, tunaamini sasa ni hatua ya kusogea mbele tuachane na yaliyopita”
Mr II alifunga mjadala kwa kuamplfy zaidi kwamba “ni kweli tulikua katika vita na vita lazima ifike mwisho labda iwe ni vita isiyo na malengo ndio haitaki suluhu lakini kama ilikua na malengo ina maana inapopatikana fursa ya suluhu kama kweli ulikua na dhamira a dhati kwa kile unachokipigania lazima ukubali kukaa chini na kutafuta suluhu ili tusonge mbele, tumekubaliana, sasa tunasonga mbele na wengine sasa hivi tupate fursa sasa hivi kujikita zaidi kwenye siasa za kitaifa”

Sunday, February 19, 2012

DK. MWAKEMBE AMJIBU DCI MANUMBA!


 Dk. Harrison G Mwakyembe

           Dk. Harrison G. Mwakyembe (Mb), NW-UJ
Dar es Salaam
18/02/12
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nimelazimika leo Jumamosi, tarehe 18 Februari, 2012 kutoa taarifa hii kwa vyombo vya habari kufuatia mkutano wa DCI Robert Manumba na waandishi wa habari jana (17/02/12) kuongelea, pamoja na mambo mengine, hali yangu ya afya na kuhitimisha, kienyejienyeji tu kuwa “sikunyweshwa sumu” ila naumwa tu ugonjwa wa ngozi bila kufafanua ugonjwa huo wa ngozi umesababishwa na nini!
Napenda nisisitize mapema kabisa kuwa msimamo huo wa Jeshi la Polisi umenikera sana katika hali niliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake unaoendelea hospitali ya Apollo nchini India ambako bado sijahitimisha matibabu yangu; pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu; na tatu kwa Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.
Itakumbukwa kuwa tarehe 9 Februari, 2011 nilimwandikia barua IGP Said Mwema kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa maisha yangu na ya viongozi wengine. Kwa kutambua kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania daima husisitiza kuletewa ushahidi kwanza ndipo lifanyekazi, nilihakikisha nimeainisha katika barua  hiyo kila ushahidi nilioupata au kupewa. (Utaratibu huu wa Jeshi la Polisi kusubiri kuletewa ushahidi mezani, kama ambavyo mahakimu wanavyosubiri ushahidi mahakamani, haupo popote pale duniani (ila Tanzania tu) kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni kutafuta ushahidi. Polisi wanachohitaji duniani kote ni kupata clue au tetesi tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika). Pamoja na kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi niliokuwa nao, mambo manne yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na dhamira ya dhati ya kupeleleza suala hilo:
(i)                Siku chache baada ya kumkabidhi IGP barua hiyo, nilitumiwa timu ya “wapelelezi” ofisini kwangu kuja kuchukua maelezo yangu ya ziada. Timu hiyo ilikuwa inaongozwa na ACP Mkumbo, afisa wa polisi ambaye wiki chache zilizokuwa zimepita alikuwa miongoni mwa askari waliotuhumiwa kupokea rushwa kwa lengo la kumbambikizia madawa ya kulevya mtoto wa Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, suala ambalo mpaka leo hii uongozi wa Polisi umeshindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Kwa msingi huo, nilikuwa nimeletewa mtuhumiwa wa rushwa/ ujambazi kuendesha uchunguzi wa watuhumiwa wengine wa ujambazi! Nikatambua mara moja kuwa zoezi zima lilikuwa la mzaha, tena mzaha mkubwa!
(ii)              Wiki chache baada ya barua yangu kuwasilishwa kwa IGP na timu ya ACP Mkumbo “kuanza kazi”, Jeshi la Polisi likachukua hatua ya kuwapongeza na kuwazawadia askari niliowatuhumu kushirikiana na majambazi! Huhitaji kuwa profesa wa falsafa kuelewa kuwa huo ulikuwa ujumbe tosha wa kunipuuza.
(iii)            Hivi karibuni tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya ujambazi mkoani Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari “wale wale” niliowatuhumu kwenye barua yangu, IGP alichukua hatua ya kuwahamishia mikoa mingine!
(iv)           ili kunikatisha tamaa kabisa, barua yangu ya “siri” kwa IGP ikavujishwa kwa makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama habari ambayo ilikebehi na kukanusha taarifa nzima niliyotoa, sijui kwa faida ya nani! Lakini huu ni mchezo wa kawaida kwa polisi kwani hivi karibuni Mhe. Waziri Samuel Sitta alipohojiwa na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi ofisini kwake, wakiwa wawili tu, taarifa ya kikao hicho ikawa kwenye moja ya magazeti ya mafisadi ikikebehi ushahidi aliotoa Sitta! The integrity of the police force leadership is on the line.
Nimeelezea vizuri katika barua yangu kwa IGP kuwa kundi hilo la mauaji lilikuwa limeelekezwa kuniua kwa kutumia sumu, taarifa ambayo kwa karibu mwaka mzima Polisi hawakutaka kuifuatilia kwa sababu wanazozijua wenyewe.  Sasa huu msukumo mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama nilipewa sumu au la na kukurupuka kutoa tamko hata kabla ya kunichunguza nilivyo, kunihoji mimi na wasaidizi wangu ofisini na hata kuongea na mabingwa wa Kihindi wanaonifanyia uchunguzi, umetokea wapi?  Si ni polisi hawahawa ambao, badala ya kushukuru,  wamekuwa wakikerwa na tahadhari ambazo Waziri Sitta amekuwa akitoa ili suala hili lichunguzwe kwa kina?
Aidha napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matatibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”! Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa wandishi wa habari hakifanani kabisa na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Apollo ambayo inatamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti /kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”!
Nimesoma darasa moja Kitivo cha Sheria Mlimani na DCI Manumba. Baadaye IGP Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa sheria Mlimani. Vigogo hawa wawili wa usalama wa raia nchini hawajanitendea haki, nao wanajua. Wanajua vilevile kuwa sitakaa kimya au kumung’unya maneno come what may pale ambapo haki inakanyagwa.
Tuendelee kuombeana afya na uhai ili tutendeane haki na vilevile tuitendee nchi yetu haki kwa kuvimalizia viporo vinavyokera vya Dowans, EPA, Kagoda n.k. kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
 
Mungu Ibariki Tanzania .

HANDSOME ALIYEITIKISA KENYA-SEHEMU YA MWISHO.....

Simon Matheri Ikere
Mwili wa Simon Matheri baada ya kuuawa


Ndugu wasomaji wa Blog hii, nimekuwa nikipokea ujumbe kupitia simu yangu ya kiganjani kutoka kwa wasomaji wakinishauri kuwa nisiwe nachelewa kuweka muendelezo wa visa na stori ninazoweka humu na pia nisiwe nachelewa ku up date blog hii mara kwa mara.
Naomba nikiri kuwa, hiyo imetokana na mlundikano wa majukumu niliyo nayo kwa sasa, naomba mniwie radhi, na nitajitahidi kuweka mada mbali mbali humu kama kawaida.
Pia ningependa kuweka wazi kuwa hizi kesi au habari za kiuhalifu ninazoweka humu pamoja na ushuhuda sio habari au visa vya kufikirika bali ni habari za kweli kabisa.
Haya, sasa tuendelee ya ile habari ya kule nchini Kenya………

ILIPOISHIA…..
Kitendo cha kuchoma nyumba yake mwenyewe ambayo aliijenga kwa msaada wa baba yake, kilimuuzi sana mzazi huyo na hivyo kumfungulia mashtaka ambapo alifungwa miaka mitano jela.

ENDELEA….

Matheri alitumikia kifungo chake cha maiak mitano katika jela yenye ulinzi mkali ya Kaimiti ambayo hutumika kwa wafungwa sugu wa ujambazi. Katika kipindi ambacho alikuwa jela, huku nyuma familia yake iliishi kwa amani, ambayo hata hivyo ilitoweka mara baada ya Matheri kuachiwa huru kutokana na kumaliza kifungo chake.

Awali wazazi wake walidhani alikuwa amebadilika kitabia kutokana na kutumikia kifungo cha miaka mitanojela, kitu ambacho haikuwa sahihi. Kumbe katika kipindi hicho ambacho alikuwa akitumikia kifungo ndipo alipo alipohitimu na kuwa jambazi sugu.

Baba yake alikiri kwambanaamini mwanaye alifuzu kuwa mwizi na jambazi sugu kwa kufunzwa wakati alipokuwa katika jela ya kamiti, jela amayo hutumika kuwafunga wahalifu sugu. Baada ya kutoka jela, baba yake aliamua kumjengea mwanaye huyo nyumba mpya akiamini kwamba atakuw aamebadilika, lakini hali ilikuwa tofauti, na nyumba hiyo badaye ilikuja kuchomwa moto na na watu wenye hasira kali kutokana na kukerwa na vitendo vyake.

Alipotoka jela tu Matheri alinunua bunduki aina ya AK-47 kutoka kwa wakimbizi wa Somalia na katika hali isiyo ya kawaida, alimtishia kaka yake kwa bunduki hiyo baada ya kutofautiana katika mambo ya kawaida tu. Baada ya mkasa huo, ilibbbidi familia ilifahamishe jeshi la Polisi, ambapo Polisi walianza kumtafuta. Kama vile machale yalimcheza, Matheri alitowerka haraka sana pale nyumbani kwao na akawa anakuja pale mara chache sana tena usiku wa manane.

Pilika zake za ujambazi zilianzia katika wilaya ya Murang’a. Akiwa na washirika wake, Matheri aliendesha ujambazi katika wilaya hiyo, mpaka alipokoswakoswa kuuwawa na Polisi katika msitu mmoja ambapo walikuw awakifuatiliwa na Polisi ambao walikuwa wanatumia mbwa wa kunusa. Katika tukio hilo washirika wake wawili waliuawa nay eye aliponea chupuchupu baada ya kujitumbukiza katika mtowenye maji yaendayo kwa kasina kupotelea kusikojulikana.

Baada ya tukio hili Matheri alihamishia makazi yake katika jiji la Nairobi ambapo pia alikuwa akitoka na kuingia katika miji mikuu ya Afrika Mashariki na kufnya uharamia na kisha kutoweka kutoka mji mmoja hadi mwingineili kuwakwepa Polisi.

Katika kipindi ambacho Matheri aliendesha uharamia katika wilaya ya Murang’a, familia yake nayo haikusalimika. Mara nyingi familia hiyo ilivamiwa na wannchi wenye hasira kali na kuchomewa nyumba ili kulipiza kisasi. Mzee Ikere alidai kwamba kila wakti mtu anapovamiwa na majambazi katika miji ya Nairobi, Mombasa, Kisumu au mji wowote, Familia yake ilikuwa ikipata usumbufu mkubwa, kwani walikuwa wakipata wageni ambao huja kulipiza kisasi kwa kufanya uharibifu mkubwa ikiwa ni pamoja na kuchoma nyumba za familia hiyo.

Ilifikia mahali hata wizi mdogo mdogo wa kuku, jina la mwanye lilihusishwa na wizi huo, kitu ambacho haikuwa kweli. Tukio ambalo Mzee Ikere anasema hatalisahau ni pale aliposhambuliwa kwa mapanga na mikuki na watu wenye hasira kali ikiwa ni katika kulipiza kisasi, kiasi kwamba aliachwa na majeraha huku akivuja damu bila kupata msaada wowote kutoka kwa majirani zake. Ilitokea hata watu wenye magari waliotaka kumpa msada ili kumpeleka hospitalini walikuwa wakitishwa kwamba nao wangeshughulikiwa. Kutokana na usumbufu huo, ilibidi waombe msaada polisi ili familia hiyo ipate msaada wa ulinzi lakini hawakupata msaada huo.

Hadi kufikia mwaka 2007, jina la Simon Matheri Ikere lilikuwa likivuma nchini Kenya kutokana na uhalifu aliokuwa akiundesha yeye na genge lake. Lakini kama waswahili wanvyosema, hakuna marefu yasiyo na ncha. Ilipofika Februari 20, 2007 ukawa ndio mwisho wa mtu huyu.

Kuuawa kwa Matheri kulipokelewa kwa hisia tofauti na jamii ya Wakenya, miongoni mwao zilikuwa ni taasisi za watetezi wa haki za binadamu. Taasisi hizo ziliwashmbulia Polisi kwamba walitumia kauli ya Waziri wa Usalama wa raia, Mheshimiwa Michike vibaya. Taasisi hizo zilipinga waziwazi kuhusu kuuawa kwa Matheri na kuwashutumu Polisi kwamba hawakumtendea haki Matheri kwani alipaswa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa kama mhalifu mwingine yeyote.

Naye mama yek mzaziMatheri, Martha Wanjiru akizungumza mara baada ya kupata taarifa za kuuawa kwa mwanye na Polisi, alisema kwamba, alijua kuwa ipo siku mwanaye huyo angeuawana hatimaye siku hiyo imefika. Mama huyo alikiri kwamba ni takribani mwaka mmoja ulikuwa umepita bila ya kumwona mwanaye.

Huku akionekana kujuta, mama huiyo alisema, “Kama ningejua, mamba ya mwanangu huyu niliyemzaa miaka 30 iliyopita, ingezaa mtoto atakayekuja kuwa muuajina kuniletea usumbufu mkubwa utakaoniumiza moyoni mwangukatika maisha yangu yote, hakika nisingemzaa, lakini hilo ni jambo ambalo siwezi kulifanya.”

Mama huyo anakiri kwamba kuna wakai aliwahi kumsihi mwanaye ajisalimishe mikononi mwa Polisi, kwani hiyo ndiyo njia pekee ambayo ingepelekea kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa kwa haki, lakini mwanaye hakukubali, badala yake akaendelea na vitendo vyake vya ujambazi.

Naye mkewe Matheri, Bi Felistus Wanjiru akimwelezea mumewe, alisema kwamba Matheri alikuwa ni mpole sana na hakuwa ni mtu wa maneno mengi. Bi Wanjiru alidai kwamba katika kipindi chote alichoishi naye hakujua kwamba mumewe alikuwa ni jambazi sugu aliyekuwa akitafutwa na Polisi.

Hata hivyo hatua inayochukuliwa na Polisi nchini Kenya ya kuwauwa majambazi kama Matheri, imewagawa wakenya katika makundi mawili. Lipo kundi linaloona kama ile ilikuwa ni hatua sahihi ya kukomesha ujambazi nchini humo, na kundi jingine linaona kuwa, hiyo haikuwa ni njia sahihi ya kukomesha ujambazi.

Je, kw Polisi kuendesha mauaji ya namna hii kwa watu wanishukiwa kuwa ni majambazi sugu, hakuliweki Taifa la Kenya katika miongoni mwamnchi zinazokiuka haki za binadamu?
Je, hali hiyo haiwezi kuufanya uhalifu kuwa wa kutisha zaidi, kwani majambazi hawatosita kuuwa wakati wanapofanya uporaji, kwa sababu wanjua hata wao wakipatikana watauawa?

Hayo yote ni miongoni mwa maswali ambayo Wakenya wengi walikuwa wakijiuliza na bado wanjiuliza, na mwenye majibu ya maswali hayo ni serikali yenyewe ya Kenya

**********************Mwisho*************************

Saturday, February 18, 2012

HANDSOME ALIYEITIKISA KENYA-SEHEMU YA PILI


Ilipoishia..............
Baada ya kumuuwa Matheri Polisi katika upekuzi walioufanya katika nyumba yake walikuta bunduki aina ya AK-47 pamoja na risasi 26. Hata hivyo upo utata uliojitokeza katika taarifa zilizonukuliwa kutoka pande mbili, yaani upande wa Polisi na mke wa Matheri kwa upande mwingine.

Endelea kufuatilia kisa hiki hapa chini…………..

Kwani kwa upande wa Polisi walidai kwamba wakati wnmuuwa Matheri alitoka akiwa na bunduki aina ya AK-47 na hivyo kuwalazimisha Polisi kumuuwa ili kujihami, lakini kwa upande wa mkewe, Felister Wanjiru ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi saba wakati huo, akihojiwa na kituo cha Luninga cha KTN alidai kuwa mumewe alitoka akiwa hana silaha yoyote, tena alitoka akiwa kifua wazi akiwa amevaa kaptula, maarufu kama Bukta huku akiwa ameweka mikono yake kichwani ili kuwaonesha Polisi kwamba hakuwa na silaha yoyote, lakini kwa mshangao Polisi walimmiminia risasi mumewe na kumuuwa palepale.

Akisimulia zaidi mkasa huo katika kituo hicho cha Luninga, Wanjiru alisema kwamba siku ya tukio alikuwa amelala na mumewe chumbani, mara akasikia michakato ya miguu nje ya nyumba yao, lakini mumewe hakuonekana kwamba alikuwa na wasiwasi, baadae walisikia sauti ya Polisi waliokuwa nje ya nyumba yao wakijitambulisha na kumtaka mumewe atoke nje na ajisalimishe haraka la sivyo wataichoma nyumba moto na kuwauwa wote waliomo ndani.

Mumewealiposikia hivyo alijificha chini ya mvungu wa kitanda ili kuokoa maisha yake. Baada ya kuona kwamba Polisi wanazidi kusisitiza msimamo wao, ilibidi amsihi mumewe ajisalimishe ili kuokoa maisha ya watoto wake, kwani katika nyumba ile walikuwa yeye Wanjiru na mumewe Matheri pamoja na watoto wao 6, huku Wanjiru akiwa akiwa na ujauzito wa miezi 7.

Akizidi kusimulia, Wanjiru alisema kwamba mumewe aliamua kutii amri ya Polisi na kutoka nje huku akiwa amevaa bukta na mikono yake ikiwa nyuma ya kichwa. Alipofika nje aliamriwa apige magoti huku akiwa ameweka mikono yake nyuma ya kichwa na aache kinywa wazi , kitu ambacho alitii.

Ndipo Polisi mmoja alipomsogelea mahali alipo na kutumbukiza mdomo wa Bunduki yake kinywani mwa Matheri na kisha kuifyatua sawia, huku kila mtu akishuhudia. Katika mauaji hayo, Polisi walikiri pia kumuuwa mtu mwingine ambaye inasemekana alikuwa ni mlinzi binafsi wa Matheri {Bodyguard}. Utata wa namna Matheri alivyouawa haukusumbua vichwa vya Wakenya walio wengi, kwani kwao hiyo haikuwa ni hoja, bali cha msingi kwao ilikuwa ni kusherehekea kuuawa kwa Matheri.

Katika kijiji alichozaliwa Matheri kilichopo magharibi mwa jiji la Nairobi vituo vya Luninga nchini Kenya vilikuwa vikionesha wakazi wa kijiji hicho wakishrehekea kwa nyimbo za kuwasifia Polisi kwa ushujaa wao wa kumuuwa mtu ambaye alikuwa ni tishio kwa usalama wao na mali zao.

Hatua ya kluuawa kwa Matheri inasemekana ni katika kutii amri ya waziri wa usalama wa raia nchini Kenya, Mheshimiwa John Michuki ambaye Wakenya walimpa jina la utani la “Kimeendero” au “Crusher” ya kuwaamuru Polisi kuwauwa majambazi pale wanpoonekana kukabiliana na Polisi kwa silaha.

Simon Matheri Ikere kijana mzuri mwenye sura ya mvuto na mpole kupindukia alikuwa ni mtoto wa nane kuzaliwa akiwa ni kitinda mimba wa familia ya Mzee Peter Ikere Gichungu aliyekuwa dereva wa malori nchini humu na mkewe Martha Wanjiru, mama wa kilokole.

Kwa mujibu wa maelezo ya wazazi wake, Simon Matheri Ikere alizaliwa mwaka 1977 na katika kipindi chote cha utoto wake hakuwahi kuonesha tabia ya wizi. Tabia walioijua aliyokuwa nayo tangu utoto wake ni ile ya kuwa na hasira za ziada ambazo hawadhani kama ndio chanzo cha mtoto wao kuwa jambazi sugu.

Baba yake alisema kwamba mwanaye alishindwa kuendelea na masomo ya elimu ya msingi katika shule ya msingi Kihara akiwa darasa la sita. Mzee huyo alikiri kutojua sababu hasa ya mwanaye kuacha shule akiwa darasa la sita ili hali alikuwa na maendeleo mazuri tu shuleni.

Baada ya kumuona mwanye ameacha shule, Mzee huyo akaamua kumpeleka katika eneo la Wangige ambalo ni maarufu kwa shughuli mbalimbali za ufundi, maarufu kama Jua Kali nchini Kenya.

Matheri alipelekwa katika eneo hilo ili akajifunze ufundi wa kuchomea vyuma {Welding}. Baba yake anakiri kwamba huenda katika eneo hilo la Wangige ndipo mwanaye alipojifunza tabia ya uchomaji wa nyumba moto {Arsonist}, ingawa hata hivyo wataalamu wansema tabia hii ni maradhi.

Siku moja miaka saba iliyopita ndipo vitendo hivyo vya uchomaji nyumba moto vilipoanza pamoja na usumbufu mdogo mdogo katika familia. Mzee huyo anakumbuka siku moja likuw ametofautiana naye na kutokana na hasira zake za ziada Matheri aliamua kuchoma nyumba yake mwenyewe na kisha kutoweka.

Kitendo cha kuchoma nyumba yake mwenyewe ambayo aliijenga kwa msaada wa baba yake, kilimuuzi sana mzazi huyo na hivyo kumfungulia mashtaka ambapo alifungwa miaka mitano jela.

Ni nini kitatokea baada ya Matheri kumaliza kifungo chake….Fuatilia kisa hiki kesho

Friday, February 17, 2012

MJUE CHE GUEVARA

Che guevara
Ernesto Rafael Guevara de la Serna au Che Guevara kuzaliwa  (* 14. Mei 1928 Rosario, Argentina; kifo † 9. Oktoba 1967 La Higuera, Bolivia) alikuwa mtabibu mzaliwa wa Argentina aliyekuwa mfuasi wa itikadi za Kisoshalisti za Karl Marx. Guevara anajulikana zaidi kwa harakati zake za kimapinduzi dhidi ya tawala za kibepari huko Amerika ya Kusini na Afrika.
Wakati akisomea utabibu, Che Guevara alizunguka katika nchi mbalimbali za Marekani ya Kusini ambapo alijionea mwenyewe umasikini uliokithiri. Alisikitishwa sana na maisha ya ufukara waliokuwa wakiishi wananchi wengi huku wachache wakiwa wanamiliki mali za nchi hizo. Alifikiria jinsi ya kuweza kubadili hali hii na kuamua kuwa njia pekee ya kuondoa umasikini na ukandamizaji ni mapinduzi. Aliamua kusoma kwa undani falsafa za Karl Marx na baada ya hapo alijihusisha na harakati za kisoshalisti nchini Guatemala chini ya rais Jacobo Arbenzi Guzmán.
Mwisho mwa miaka ya 1950, Guevara aliungana na Fidel Castro aliyekuwa akiongoza kundi la kijeshi lililotwaa madaraka kwa nguvu nchini Kuba mwaka 1959. Guevara alikuwa mmoja wa viongozi wa serikali mpya ya Kuba. Katika kipindi hiki, Guevara aliandika vitabu na makala mbalimbali kuhusu nadharia na vitendo vya vita vya msituni kwa nia ya kuondoa madarakani tawala za kibepari na kibeberu.
Mwaka 1965 Guevara aliondoka nchini Cuba akielekea Kongo-Kinshasa (hivi sasa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo) kwa siri kusaidia harakati za kuondoa utawala uliokuwa ukiongozwa na vibaraka wa mataifa ya Magharibi chini ya Mobutu Sese Seko baada ya kuuawa kwa Patrice Lumumba. Moja ya watu ambao walifanya kazi na Guevara alipokuwa nchini Kongo ni aliyekuwa baadaya rais wa nchi hiyo, Laurent Kabila.
Guevara aliondoka nchini Congo na kuelekea Bolivia ambapo alikamatwa mwaka 1967 na jeshi la Bolivia likishirikiana na majasusi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA). Baada ya kukamatwa kwake aliuawa kinyama.
Baada ya kifo chake, Guevara alichukuliwa kama nguzo ya vuguvugu la kimapinduzi ya kishoshalisti duniani. Picha yake na kofia aina ya Beret aliyopenda kuivaa vimekuwa kama alama za mapinduzi ya mrengo wa kushoto duniani

HANDSOME ALIYEITIKISA KENYA.


Jiji la Nairobi, Moi Avenue

Siku ya Jumanne ya Februari 20, 2007 ni siku ambayo haitasahauliwea na Wakenya wengi, na hasa Polisi wa nchi hiyo. Ni siku ambayo Polisi zaidi ya 100 wa nchi hiyo kutoka kwenye kitengo maalum cha kupambana na uhalifu walifanikiwa kumuua jambazi mmoja sugu na aliyekuwa akitafutwa kwa udi na uvumba aliyejulikana kwa jina la Simon Matheri Ikerealiyekuwa na umri wa miaka 30.

Akiwa bado ni kijana mmbichi wa umri wa miaka 30, Simon Matheri Ikere alikuwa ni jamabzi hatari aliyekuwa akivuma katika viunga vya jiji la Nairobi kama mzimu kiasi cha Polisi kukiwekea kichwa chake dau la shilingi za Kenya zipatazo 150,000 kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kukamatwa kwake.

Ilikuwa ni majira ya saa nane na nusu za usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne, Polisi zaidi ya 100 waliizingira nyumba ya Simon Matheri Ikere iliyokuwa katika eneo la Athi River takribani kilomita 30 Kusini, Mashariki mwa jiji la Nairobi.

Katika tukio hilo ambalo lilitawaliwa na kurushiana risasi hatimaye ilibidi Polisi wamuombe mtuhumiwa ajisalimishe kwa kutoka nje ya nyumba yake ili kunusuru maisha ya watu wengine waliokuewa ndani ya nyumba ile. Simon aliamua kujisalimisha.

Wakati anatoka nje ya nyumba yake, Polisi walimshambulia kwa risasi na kumuuwa. Polisi walifanikiwa kumuuwJambazi huyo baada ya kupata taarifa kupitia kwa raia mwema, na kwa kutumia satelaiti walifanikiwa kujua mahali alipo kupitia simu yake ya mkononi, baada ya kupata namba yake ya simu kutoka kwa raia huyo mwema.

Msemaji wa Polisi nchini Kenya Gideon Kipunjatialisema kwamba Matheri alikuwa anatuhumiwa kwa mauaji ya watu zaidi ya 18 miongoni mwao wakiwa ni daktari bingwa wa maradhi ya ukimwi {AIDS} Prof. Job Bwayo ambaye aliuawa mwanzoni mwa mwezi huo huo wa Februari pamoja na mfanyakazi wa kimishenari wa Kimarekani aitwae Lois Andersnna binti yake Zelda White.

Mauaji ya Wamarekani hao yalitokea mnamo Januari 2007 katika tukio la kupora gari ambapo inasemekana Matheri na wenzie ndiyo waliohusika. Kipunjati alikiri kwamba Polisi walikuwa na ushahidi wa kina wa kumhusisha na mauaji hayo.

Naye kamanda mkuu wa Polisi wa jiji la Nairobi Njue Njagi akizungumzia tukio hilo alisema, ‘Leo ni siku kubwa kwa upande wa jeshi la Polisi, kwani tumefanikiwa kumuua jambazi sugu aliyekuwa akilisumbua jeshi la Polisi kwa muda mrefu.

Kamanda Njagi aliendelea kusema, ‘Mtu huyu alichukulia kuuwa kama kitu cha kufurahisha [hobby} lakini kwa uwezo wa Mungu leo polisi tumeweza kuzima vitendo vyake.’ Kmanda huyo aliendelea kubainisha kwamba Jeshi la Polisi bado linaendelea kuwasaka majambazi wengine watano ambao ni washirika wakuu wa Matheri.

Polisi wa nchini Kenya wanaamini kwamba Matheri alikuwa akiongoza genge la majambazi ambalo lilikuwa likiendesha uharamia katika miji mikuu ya Afrika Mahsriki, ambapo wakazi wa miji hiyo kwa muda mrefu wamekuwa majeruhi wa vitendo vya ujambazi vilivyokuwa vikiendeshwa na Matheri pamoja na genge lake.

Baada ya kumuuwa Matheri Polisi katika upekuzi walioufanya katika nyumba yake walikuta bunduki aina ya AK-47 pamoja na risasi 26. Hata hivyo upo utata uliojitokeza katika taarifa zilizonukuliwa kutoka pande mbili, yaani upande wa Polisi na mke wa Matheri kwa upande mwingine

Ni utata gani huo, fuatilia kisa hiki kesho…………..