Dar es Salaam
18/02/12
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nimelazimika
leo Jumamosi, tarehe 18 Februari, 2012 kutoa taarifa hii kwa vyombo
vya habari kufuatia mkutano wa DCI Robert Manumba na waandishi wa
habari jana (17/02/12) kuongelea, pamoja na mambo mengine, hali yangu
ya afya na kuhitimisha, kienyejienyeji tu kuwa “sikunyweshwa sumu” ila
naumwa tu ugonjwa wa ngozi bila kufafanua ugonjwa huo wa ngozi
umesababishwa na nini!
Napenda
nisisitize mapema kabisa kuwa msimamo huo wa Jeshi la Polisi umenikera
sana katika hali niliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato
wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake unaoendelea
hospitali ya Apollo nchini India ambako bado sijahitimisha matibabu
yangu; pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la
Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si
lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu;
na tatu kwa Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban
mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au
kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.
Itakumbukwa
kuwa tarehe 9 Februari, 2011 nilimwandikia barua IGP Said Mwema
kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa maisha yangu na ya viongozi wengine.
Kwa kutambua kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania daima husisitiza kuletewa
ushahidi kwanza ndipo lifanyekazi, nilihakikisha nimeainisha katika
barua hiyo kila ushahidi nilioupata au kupewa. (Utaratibu huu wa Jeshi
la Polisi kusubiri kuletewa ushahidi mezani, kama ambavyo mahakimu
wanavyosubiri ushahidi mahakamani, haupo popote pale duniani (ila
Tanzania tu) kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni kutafuta
ushahidi. Polisi wanachohitaji duniani kote ni kupata clue
au tetesi tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika).
Pamoja na kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi niliokuwa nao, mambo
manne yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na
dhamira ya dhati ya kupeleleza suala hilo:
(i) Siku
chache baada ya kumkabidhi IGP barua hiyo, nilitumiwa timu ya
“wapelelezi” ofisini kwangu kuja kuchukua maelezo yangu ya ziada. Timu
hiyo ilikuwa inaongozwa na ACP Mkumbo, afisa wa polisi ambaye wiki
chache zilizokuwa zimepita alikuwa miongoni mwa askari waliotuhumiwa
kupokea rushwa kwa lengo la kumbambikizia madawa ya kulevya mtoto wa
Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, suala ambalo mpaka leo hii uongozi wa
Polisi umeshindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Kwa msingi huo,
nilikuwa nimeletewa mtuhumiwa wa rushwa/ ujambazi kuendesha uchunguzi wa
watuhumiwa wengine wa ujambazi! Nikatambua mara moja kuwa zoezi zima
lilikuwa la mzaha, tena mzaha mkubwa!
(ii) Wiki
chache baada ya barua yangu kuwasilishwa kwa IGP na timu ya ACP Mkumbo
“kuanza kazi”, Jeshi la Polisi likachukua hatua ya kuwapongeza na
kuwazawadia askari niliowatuhumu kushirikiana na majambazi! Huhitaji
kuwa profesa wa falsafa kuelewa kuwa huo ulikuwa ujumbe tosha wa
kunipuuza.
(iii) Hivi
karibuni tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya ujambazi
mkoani Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari “wale wale”
niliowatuhumu kwenye barua yangu, IGP alichukua hatua ya kuwahamishia
mikoa mingine!
(iv) ili
kunikatisha tamaa kabisa, barua yangu ya “siri” kwa IGP ikavujishwa
kwa makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama habari ambayo
ilikebehi na kukanusha taarifa nzima niliyotoa, sijui kwa faida ya
nani! Lakini huu ni mchezo wa kawaida kwa polisi kwani hivi karibuni
Mhe. Waziri Samuel Sitta alipohojiwa na ofisa mwandamizi wa Jeshi la
Polisi ofisini kwake, wakiwa wawili tu, taarifa ya kikao hicho ikawa
kwenye moja ya magazeti ya mafisadi ikikebehi ushahidi aliotoa Sitta! The integrity of the police force leadership is on the line.
Nimeelezea
vizuri katika barua yangu kwa IGP kuwa kundi hilo la mauaji lilikuwa
limeelekezwa kuniua kwa kutumia sumu, taarifa ambayo kwa karibu mwaka
mzima Polisi hawakutaka kuifuatilia kwa sababu wanazozijua wenyewe.
Sasa huu msukumo mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama nilipewa
sumu au la na kukurupuka kutoa tamko hata kabla ya kunichunguza
nilivyo, kunihoji mimi na wasaidizi wangu ofisini na hata kuongea na
mabingwa wa Kihindi wanaonifanyia uchunguzi, umetokea wapi? Si ni
polisi hawahawa ambao, badala ya kushukuru, wamekuwa wakikerwa na
tahadhari ambazo Waziri Sitta amekuwa akitoa ili suala hili lichunguzwe
kwa kina?
Aidha
napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa
halisi ya matatibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na kama
waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”! Nasema hivyo kwa kuwa
alichokisema DCI Manumba kwa wandishi wa habari hakifanani kabisa na
picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Apollo ambayo inatamka wazi kuwa
kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo,
kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti /kukiondoa
huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila
msingi wa kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”!
Nimesoma
darasa moja Kitivo cha Sheria Mlimani na DCI Manumba. Baadaye IGP
Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa sheria Mlimani. Vigogo hawa wawili wa
usalama wa raia nchini hawajanitendea haki, nao wanajua. Wanajua
vilevile kuwa sitakaa kimya au kumung’unya maneno come what may pale ambapo haki inakanyagwa.
Tuendelee
kuombeana afya na uhai ili tutendeane haki na vilevile tuitendee nchi
yetu haki kwa kuvimalizia viporo vinavyokera vya Dowans, EPA, Kagoda
n.k. kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania .
No comments:
Post a Comment