Jengo la Hospitali ya Royal Derby Sunday, February 01, 2009 7:51 AM
Wafanyakazi katika hospitali mpya ya kisasa katika mji wa Derby nchini Uingereza wamelalamikia kutishika kutokana na majini na mizuka inayofanya vitu vya ajabu ajabu katika hospitali hiyo. Wafanyakazi katika hospitali hiyo wamekuwa wakilalamika kuona vitu vya ajabu ajabu katika korido za hospitali ya Royal Derby ambayo ujenzi wake umegharimu mamilioni ya pound.

Mmoja wa wafanyakazi hao alisema "Mzuka wa Mwanaume aliyevaa nguo nyeusi unachomoza na kupotea kutoka katika kuta za korido za hospitali hiyo" alisema mfanyakazi huyo na kuongeza kuwa mizuka hiyo inatokeza kwa wingi karibu na chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.

Kutokana na hali hiyo inasemekana mchungaji mmoja ameombwa aende kwenye hospitali hiyo akafanye sala za kufukuza majini hayo.

Uongozi wa hospitali hiyo ulisema kuwa unayachukulia malalamiko ya wafanyakazi hao kwa uangalifu zaidi na kusema haina mpango wa kufanya kafara au maombi katika hospitali hiyo.

Mchungaji Canon Elaine Jones wa Derby amekiri kuombwa kwenda kufanya maombi ya kufukuza majini yanayozunguka katika hospitali hiyo.

Mji wa Derby inasemekana unaongoza kwa kuwa na mizuka na majini wengi kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mtafiti wa masuala hayo Lionel Fanthorpe.

Utafiti huo ulionyesha kuwepo kwa majini na mizuka 315 katika mji huo.