TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kampeni ya kupunguza umri wa urais haina uhusiano na mimi kutaka kugombea urais 2015
1.
Baadhi ya vyombo vya habari vimehusisha kauli yangu ya kutaka
kupunguza umri wa kugombea urais na mimi ‘kuutaka urais’. Mimi nikiwa
mwanachama na kiongozi wa chama chama changu cha CHADEMA naelewa na
kuziheshimu taratibu na kanuni tulizojiwekea za kuomba nafasi mbalimbali
za uongozi, ikiwemo nafasi ya urais. Nafasi ya uongozi ndani ya CHADEMA
haiombwi kwenye warsha. Iwapo chama change, wakati muafaka ukifika na
kutokana na matakwa ya jamii, kikiona nipewe jukumu lolote sitasita
kutekeleza wajibu huo niwe au nisiwe mgombea.
2.
Kwa hivyo, nilichozungumza jana ni kutoa maoni yangu kwamba muda
umefika kwa Taifa letu kupunguza umri wa kugombea urais. Maoni yangu
haya yanatokana na ukweli kwamba hakuna sababu zozote za kisayansi
zinazomfanya mtu aliye chini ya umri wa miaka 40 akose sifa za kuwa
Rais. Msimamo huu nimekuwa nao tangu zamani nikisoma shule na haujawahi
kubadilika. Hakuna mahala popote katika maoni yangu niliyotoa jana
niliposema kwamba nataka umri wa urais upunguzwe ili nipate fursa ya
kugombea nafasi ya urais. Pia siwezi kutaka katiba iandikwe kwa ajili
yangu. Vilevile kamwe isionekane kwamba matakwa ya muda mrefu ya vijana
ya kutaka umri wa kugombea Urais kupunguzwa yanalenga kunipa fursa mimi
kwani mimi ni binaadamu naweza nisiwe na sifa za kuwa Rais lakini kukawa
na vijana wengine wengi wenye umri chini ya miaka 40 wenye Uwezo na
Uzalendo wa kutosha kushika usukani wa nchi yetu. Ni maoni yangu kwamba
tupate mabadiliko ya vizazi katika uongozi wa nchi yetu ili kukabili
changamoto za sasa zinazokabili Taifa letu.
3.
Tunapojiandaa kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya ni vizuri vyombo vya
habari vikajikita kutoa taarifa bila kuweka tafsiri au kuwatafasiria
maoni ambayo wananchi na viongozi watakuwa wanayatoa kuhusu maudhui ya
Katiba Mpya.
No comments:
Post a Comment